• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:40 PM
Jagina wa soka Diego Maradona aaga dunia akiwa na umri wa miaka 60

Jagina wa soka Diego Maradona aaga dunia akiwa na umri wa miaka 60

Na MASHIRIKA

JAGINA wa soka raia wa Argentina, Diego Maradona ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 60.

Nguli huyo ambaye pia aliwahi kuwa mkufunzi amefariki baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye ubongo mapema katika mwezi wa Novemba, 2020.

Wakati huo, ilitangazwa kwamba angetibiwa kwa tatizo la uraibu wa vileo na dawa za kulevya.

Akiwa miongoni mwa wanasoka bora wa muda wote, Maradona alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Argentina iliyonyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 1986, akibeba kikosi hicho kutokana na utajiri wa kipaji chake cha kutoka mabeki kirahisi, kupiga chenga za maudhi na kutikisa nyavu wa wapinzani kirahisi.

Wakati enzi yake ya uchezaji katika kiwango cha klabu, Maradona aliwasakatia Barcelona nchini Uhispania na Napoli aliowashindia mataji mawili ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Maradona alifunga jumla ya mabao 34 kutokana na mechi 91 ndani ya jezi za timu ya taifa ya Argentina ambayo aliiwakilisha kwenye fainali nne za Kombe la Dunia.

Maradona alikuwa sehemu ya kikosi cha Argentina kilichotinga fainali ya Kombe la Dunia nchini Italia mnamo 1990 na wakazidiwa maarifa na Ujerumani.

Aliiwakilisha tena timu yake hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia za 1994 nchini Amerika akiwa nahodha. Hata hivyo, alilazimika kutumwa nyumbani baada ya kupatikana na chembechembe nyingi za dawa haramu aina ya ephedrine kwenye vipimo vya damu.

Katika kipindi cha pili cha taaluma yake ya usogora, Maradona alihangaika sana na athari za matumizi ya dawa za kulevya aina ya cocaine na akapigwa marufuku ya miezi 15 baada ya kupatikana na tatizo la utegemezi wa dawa za kulevya mnamo 1991.

Maradona alistaafu rasmi soka ya kitaaluma akichezea kikosi cha Boca Juniors cha Argentina mnamo 1977 akiadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa.

Baada ya kuwa kocha wa vikosi viwili vya soka nchini Argentina, Maradona aliteuliwa kuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya Argentina mnamo 2008 na akaagana na kikosi hicho mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Afrika Kusini mnamo 2010. Argentina walibanduliwa na Ujerumani katika hatua ya nane-bora kwenye fainali za kipute hicho.

Hadi kifo chake, Maradona aliyewahi pia kudhibiti mikoba ya vikosi mbalimbali katika Milki za Falme za Kiarabu (UAE) na Mexico, alikuwa mkufunzi wa kikosi cha Gimnasia Esgrima katika Ligi Kuu ya Argentina.

Miongoni mwa wanadimba maarufu waliomwomboleza Maradona ni nyota wa zamani wa soka nchini Brazil, Edson Arantes do Nascimento almaarufu Pele aliyesema, “Siku moja tutasakata soka mbinguni”.

You can share this post!

Mvua kiwango kilichopitiliza kunyesha nchini, idara ya...

Morans wang’atwa na ‘The Lions’ ya Senegal mechi za...