JAMES GIKONYO: Malofa wajiunge na karate
Nan LAWRENCE ONGARO
MWANAKARATE James Mwangi Gikonyo wa klabu ya NSSF Nairobi, amejitolea vilivyo kucheza mchezo huo bila kurudi nyuma.
Anasema alijiunga na mchezo wa karate mwaka wa 2001 akiwa bado kijana wa miaka 16 lakini sasa amebobea vilivyo kwa mchezo huo na kuweza kupata mkanda mweusi wa 2nd Dan.
“Kufikia kiwango hicho kunahitaji mchezaji kujitolea mhanga kwani inataka kujituma na kuweka nidhamu mbele,” alisema Gikonyo.
Anamsifu mkufunzi wake wa jadi Bon Awiti, ambaye pia ndiye kocha mkuu wa timu ya karate nchini.
“Ningetaka kuwashauri vijana chipukizi wanaojiunga na karate wawe wanyenyekevu. Jambo muhimu ni kufuata maagizo ya kocha wako na uvumilie yote unayoagizwa kufanya,” alisema Gikonyo.
Katika mashindano ya Afrika ya karate yaliyofanyika Afrika kusini mwaka jana wa 2018, aliweza kupata nafasi ya 5 huku nchi zipatazo 25 zikishiriki.
Anasema licha ya kucheza mchezo huo wa karate ameoa na mkewe pia ni mwanakarate huku wakiwa wamejaliwa watoto wawili.
“Ninafurahi mke wangu akiwa mwana karate kama mimi kwa sababu sisi sote tumedumisha nidhamu ya hali ya juu katika nyumba yetu ambapo hakuna migogoro ambayo hushuhudiwa na waliooana.
Anasema kile kinachoponza mchezo wa karate kuendelea zaidi ni kukosa udhamini wa kutosha
“Iwapo kungekuwa udhamini wa kutosha na kikosi cha Kenya iweze kupata nafasi kusafiri nje kila mara, bila shaka kutakuwa na mabadiliko makubwa ,” alisema Gikonyo.
Kwa wakati huu mwana karate huyo anaendelea na mazoezi makali huku lengo lake kuu likiwa ni kushiriki mashindano ya karate nchini Botswana. Pia kuna mashindano mengine yatakayofanyika Afrika Kusini .Mashindano hayo ni ya ufuoni mwa bahari ya (Africa Beach Games).Mashindano mengine mwaka huu ni yale ya Zone 5 ANOCA Youth Games yatakayoandaliwa Kigali, Rwanda.
Kuna mashindano mengine ya Afrika yatakayofanyika Morocco. Halafu mashindano ya Olimpiki ya 2020 yanangojewa na hamu huku yakitarajiwa kufanyika mjini Tokyo, Japan.
Anasema jambo lingine linaloponza juhudi za mchezo huo kuendelea ni siasa miongoni mwa maafisa wanaosimamia mchezo huo.
“Iwapo mambo yangeendeshwa kwa njia inayostahili bila shaka mchezo huo unaweza piga hatua kubwa,” alisema na kuongeza washika dau wote wanaostahili kuendesha mchezo huo wanastahili kuja pamoja na kuamua mwelekeo unaostahili.
Anatoa mwito kwa vijana popote walipo wajiunge na mchezo wa karate kwa minajili ya kujiendeleza kimichezo.
“Vijana wengi malofa wanastahili kujiunga na mchezo wa karate kwa sababu mchezo huo unafunza mtu kuwa na maadili mema pamoja na nidhamu ya hali ya juu.”