• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Jasiri: Mabingwa wa Mombasa Open wajiandaa kwa Mashindano ya Dunia

Jasiri: Mabingwa wa Mombasa Open wajiandaa kwa Mashindano ya Dunia

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MASHINDANO ya Makala ya 11 ya Mombasa Open Tong-IL Moo-Do International Championship yaliyomalizika Desemba 2023, yamethibitisha jinsi Kenya inavyouchukulia mchezo huo kuwa wa muhimu. 

Wakati wa mashindano hayo yaliyoanza Desemba 15 na kumalizika Desemba 19, 2023, timu ya taifa almaarufu ‘Jasiri’, ilithibitisha kuwa itaendelea kuwa mojawapo ya timu zitakazotamba kwenye mashindano yoyote ya kimataifa.

Kuthibitisha hivyo ni wakati wa mashindano ya dunia ya mchezo hiyo yaliyofanyika huko Chung-Ju nchini Korea Kusini ambapo Jasiri ilikamilisha mashindano hayo ikiwa katika nafasi ya pili, ikishindwa kwa medali moja pekee na wapinzani wao wa jadi Ufilipino.

Kwenye mashindano ya Mombasa Open ya Makala ya 11, Jasiri ambayo imetawala mashindano hayo tangu yaanzishwe miaka 10 iliyopita, ilifanikiwa kushinda kwa medali nyingi zaidi ya makala mengine yote kwa kupata nishani za dhahabu 46, nazo za fedha 52 kisha za shaba 93 ambapo kwa ujumla ilizoa medali 191.

Salma Ali (kulia) wa timu ya Jasiri akimuelemea Djimadoum Simyeon wa Zambia wakati wa pigano lao la kitengo cha Sparring kwa wanawake wa uzani wa kilo 80-89. Salma alishinda medali ya dhahabu. PICHA | ABDULRAHMAN SHERIFF

Mwenyekiti wa Shirikisho la Tong-IL Moo-Do la Kenya (KTIMDF), Clarence Mwakio ameshukuru wale wote waliofanikisha mashindano hayo wakiwemo maafisa wa serikali waliohakikisha udhamini unapatikana kwa wakati, wadhamini wote, vyombo vya habari, wachezaji na maofisa wote wa shirikisho hilo.

“Hatuna budi kumshukuru Waziri wa Michezo Ababu Namwamba, na Katibu wa Wizara ya Michezo Peter Tum kwa kuhakikisha tumesaidika na mashindano yamemalizika kwa mafanikio makubwa,” akasema Mwakio.

Kinara huyo amesema wanatafuta washirika wa kujitolea kutoa ufadhili kwa wanamichezo wapate kuendeleza masomo ya elimu ya juu.

Alisema kuwasaidia wanachama wao kufuata elimu ya juu ni sehemu muhimu ya mikakati yao ya muda mrefu ili kuongeza ujuzi na uwezo wa wanamichezo wao.

“Mambo ya elimu iko ndani ya moyo wangu. Kwa kutoa fursa za elimu zaidi ndani ya mchezo, shirikisho sio tu kuwekeza katika mustakabali wa wachezaji wake bali pia ukuaji na maendeleo ya mchezo kwa ujumla. Kwa kuzingatia elimu, tunalenga kuwawezesha wachezaji wetu wawe wanamichezo bora wenye elimu,” alisema.

Alisema wako wanariadha kadhaa wa mchezo huo wa Tong-IL Moo-Do ambao wamehitimu kuwa wakufunzi na tayari wanatoa utajiri wao wa maarifa na ujuzi kwa wale wanaoanza kujiunga na mchezo huo.

“Timu yetu ina wanariadha wachanga na wenye uzoefu na pia itasaidia vipaji vingine vijavyo. Hii ndiyo njia ya kukuza mchezo,” alisema Mwakio.

Maafisa wa Shirikisho la Tong-IL Moio-Do la Kenya (KTIMDF) wakiongozwa na mwenyekiti wake Clarence Mwakio (wa nne kushoto) wawahutubia wanahabari kuhusu kukamilika kwa maandalizi yao. PICHA | ABDULRAHMAN SHERIFF

Nahodha wa timu ya Jasiri, Elvis Malipe, amesema kuwa wachezaji wanaendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya kujitayarisha kwa mashindano ya World Tong-IL Moo-Do Championship yatakayofanyika jijini Manila nchini Ufilipino kuanzia Oktoba 19, 2024, hadi Novemba 3, 2024.

“Tuna imani kubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kwani ikifika wakati huo, tutakuwa tumeiva kwa mazoezi na hatutatishwa na wachezaji wa nchi yoyote,” akasema Malipe.

Malipe amesema wapinzani wao wakubwa katika mchezo huo ni Ufilipino, wenyeji wa mashindano hayo. Ingawa hivyo, anaamini watahitajika kujiandaa mapema ili waweze kuwapiku wapinzani wao hao.

“Tuna imani kubwa kama tutaanza matayarisho ya mapema ya kukiandaa kikosi chetu, basi hakuna litakalotufanya tusirudi nyumbani na ushindi mkubwa. Tuna wachezaji wengi ambao hivi sasa wana uzoefu hasa kwa kushiriki mashindano ya Mombasa Open,” akasema nahodha huyo.

Kwa upande mwingine, KTIMDF ina mipango ya kuueneza mchezo huo mashinani na hasa kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu.

“Tunaamini mchezo ukishika kasi shuleni, tutakuwa na wanamichezo wengi mahiri,” amesema Mwakio.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa kidini washangaa vijana kulewa licha ya kulia...

Raila kwa Ruto: Umevuka mstari mwekundu

T L