Michezo

Jepkosgei amezea kuvunja rekodi ya mbio za marathon

November 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MWANARIADHA Joyciline Jepkosgei amefichua azma ya kuvunja rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 42 baada ya kuibuka mshindi wa New York Marathon, Amerika mnamo Jumapili.

Rekodi ya dunia katika mbio za marathon kwa sasa inashikiliwa na Mkenya Brigid Kosgei ambaye amepania kubadilisha uraia na kuanza kupeperusha bendera ya Amerika baada ya Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mwaka ujao.

Jepkosgei ambaye kwa sasa ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 21, alikuwa akishiriki mbio za marathon kwa mara ya kwanza. Alikamilisha mbio za wikendi iliyopita kwa muda wa saa 2:22:38 mbele ya Mkenya mwenzake Mary Keitany aliyeandikisha muda wa saa 2:23:32.

Ruti Aga wa Ethiopia aliambulia nafasi ya tatu baada ya muda wa saa 2:25:51.

Kwa upande wa wanaume, Mkenya Geoffrey Kamworor aliibuka mshindi wa marathon kwa mara ya pili chini ya kipindi cha miaka mitatu. Kamworor alimpiku Mkenya mwenzake Albert Korir aliyeridhika na nafasi ya pili.

Mtimkaji alikamilisha mbio za Jumapili uwanjani Central Park baada ya muda wa saa 2:08:13 na kukumbatiwa na bingwa wa Olimpiki na Dunia Eliud Kipchoge, ambaye amekuwa akifanya naye mazoezi ya pamoja.

Mwethiopia Lelisa Desisa aliyekuwa akitetea ubingwa wa taji lake alijiondoa katika hatua ya kilomita saba, siku 29 baada ya kutawazwa bingwa wa dunia katika riadha zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar.

Istanbul Marathon

Kwingineko, Mkenya Daniel Kipkore Kibet aliibuka mshindi wa makala ya 41 ya Istanbul Marathon nchini Uturuki baada ya kuandikisha muda wa saa 2:07:41.

Muda huo ndio wa kasi zaidi kuwahi kusajiliwa katika historia ya mbio hizo zilizowaleta pamoja zaidi ya wanariadha 37,000 kutoka nchi 63 tofauti wikendi iliyopita.

Kibet aliwazima kirahisi Mkenya Elias Kemboi Chelimo aliyeibuka bingwa mnamo 2015, Evans Kiplagat wa Azerbaijan aliyetwaa ufalme mnamo 2016, Mfaransa Abraham Kiprotich aliyeibuka mshindi mnamo 2017 na Felix Kimutai wa Kenya ambaye alinyanyua taji la mwaka 2018.

Yitayal Atnafu Zerihun wa Ethiopia alikamilisha mbio hizo kwa upande wa wanaume katika nafasi ya pili baada ya kuandikisha muda wa saa 2:09:44 mbele ya Mkenya Peter Kwemoi Ndorobo aliyeridhika na nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:10:09.

Kwa upande wa wanawake, Hirut Tibebu wa alizitawala mbio hizo kwa muda wa saa 2:23:40 mbele ya Mwethiopia mwenzake Tigist Abayechew aliyeandikisha muda wa saa 2:24:15. Maurine Chepkemoi wa Kenya aliambulia nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:26:02.

Katika mbio za kilomita 21, Mkenya Mathew Kimeli aliibuka mshindi huku taji la wanawake likinyanyuliwa na Tsigie Gebreselama aliyempiku Mwethiopia mwenzake Fatuma Sado ambaye aliambulia nafasi ya tatu mnamo 2018.