• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Jericho Allstars msimu huu imeona giza ligi ya S8PL

Jericho Allstars msimu huu imeona giza ligi ya S8PL

Na JOHN KIMWERE

KINYANG’ANYIRO cha kufukuzia taji la Super Eight Premier League (S8PL) kinaendelea kusababisha vita vya ubabe baina ya mahasimu wakuu msimu huu.

Ushindani unaoendelea kushuhudiwa kati ya timu za Githurai Allstars, Meltah Kabiria, Chuo Kikuu cha Kiufundi cha TUK bila kuweka katika kaburi la sahau mabingwa watetezi, Jericho Allstars hakika unatetemesha washiriki wengine.

”Bila kujipigia debe wala kusifia kampeni za soka la msimu huu zimeibuka tete kinyume na ilivyokuwa muhula uliyopita,” anasema kocha wa Jericho Allstars, Thomas Okongo na kuongeza kuwa hadi sasa ni vigumu kubashiri timu itakayomaliza kileleni na kutawazwa mabingwa.

Anasema huenda mechi za mwisho ndizo zitakazoamua bingwa wa michuano ya msimu huu.

Tangu mechi hizo zianze timu hizo nne zimekamatiana shingo ni kama kwamba hakuna mkali baina yazo kila moja ikitafuta ubabe wa kutawazwa wafalme wa ngarambe hiyo.

Kwenye jedwali ya michezo hiyo, mahasimu hao wameketi sako kwa bako tofauti ikiwa pengine pointi moja ama mbili au idadi ya mabao.

”Zimesalia takribani mechi sita kukamilisha ratiba yetu ambapo tumepania kushiriki kila moja kama fainali kwa kuzingatia kamwe hakuna mpinzani wa kupuuza. Kando na upinzani tunaozidi kushuhudia baina yetu tunaotikisa kampeni za msimu huu nyakati zingine tunaandikisha matokeo tofauti ambapo hakli hiyo inaashiria kipute cha muhula huu siyo rahisi,” alisema.

Kocha huyo anadai kuwa licha ya kukosa huduma za wachezaji sita kikosi chake kimekaa thabiti kujikaza kisabuni na kuhifadhi taji hilo.

Imebainika kuwa vijana hao wamejiunga na timu zinazoshiriki soka la Supa Ligi ya Taifa (NSL) msimu huu. Wapigagozi hao wakiwa ni Simon Namswa, Kevin Ndung’u na Alex Kakindu wote (Mt Kenya United) pia Mackbul Abdul Karim (Modern Coast FC). Pia wapo Dismas Odhiambo na Bramwel Kavaya wanaopigia Fortune Sacco na FC Talanta mtawalia.

Mtihani mgumu

Jericho ina mtihani mgumu baada ya kuzimwa na Makadara J.S.L.A mara mbili kwa mabao 4-1 na mabao 2-0 kwenye mechi ya mkumbo wa kwanza na raundi ya pili mtawalia. Jericho ambayo huchezea mechi za ligi Uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi inalenga kukazana kiume itakapoteremka katika ardhi ya nyumbani kushiriki mechi tano kati ya sita zilizosalia. Katika ratiba hiyo, timu hiyio itatifua vumbi dhidi ya RYSA, itamenyana na Mathare Flames, itakabili Metro Sports, itapambana na TUK kisha itapatana na Shaurimoyo Sportiff. Kwenye mechi ya ugenini itazuru mtaani Huruma kucheza na Huruma Kona.

Hawa ndiyo baadhi ya wachezaji wa Jericho Allstars: Raphael Ndakuwe, Calvin Onguro, Brian Kariuki, Kevin Oloo, Rrian Ochieng, Zangi Mwangi, Brian Kasasi, Ryan Odhiambo, George Oduor na Philip Kimone kati ya wengine.

Kwenye jedwali ya kinyang’anyiro hicho Githurai Allstars imetwaa usukani kwa alama 43, sawa na Jericho Allstars baada ya kucheza mechi 23 na 24 mtawalia. Nayo Meltah Kabiria imetinga tatu bora kwa kufikisha pointi 42, moja mbele ya TUK kutokana na mechi 22 na 24 mtawalia. Baada ya MASA kuandikisha alama 40 kwa kucheza mechi 24 inakamata tano bora.

Kidumbwedumbwe hicho pia kinajumuisha timu 16 zingine zikiwa: Mathare Flames, Dagoretti F.P, NYSA, Team Umeme, Metro Sports, Huruma Kona, Shaurimoyo Sportiff, Lebanon FC, Rongai All Stars, Makadara J.L.S.A na Kawangware United.

  • Tags

You can share this post!

KIU YA UFANISI: Wengi hustaajabia kuku wake walao mboga na...

KAMAU: Ufisadi nchini umegeuka zimwi litakalomeza wote

adminleo