Michezo

Jericho Allstars na South B United kuwasha moto Chapa Dimba

April 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wavulana ya Jericho Allstars itapepetana na South B United katika fainali ya Mkoa wa Nairobi kuwania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two, baada ya kufanya kweli kwenye nusu fainali zilizochezewa uwanja wa Goan Institute Pangani Nairobi.

Waliokuwa mabingwa watetezi, Gor Mahia Youth ilibanduliwa katika makundi. Baada ya malkia wa mwaka uliyopita, Beijing Raiders kuondolewa katika makundi itakuwa zamu ya Carolina for Kibera kuvaana na Acakoro Ladies kusaka taji hilo pia tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za kitaifa.

South B United ya kocha, John Mandela ilinasa tiketi ya fainali ilipokomoa Uweza FC kwa mabao 2-0 nayo Jericho Allstars ilivuna ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Brightstar Academy.

South B United iliyoshusha mchezo safi ilibeba mafanikio hayo kupitia Enock Wanyama na Victor Madengwa wapocheka na wavu mara moja kila mmoja.

Naye Bramwell Kavaya alitikisa wavu mara mbili na kusaidia Jericho Allstars kutwaa ushindi huo huku Collins Ambayo akitingia Brightstar bao la kufuta machozi.

Okisa Elkite wa Dagoretti FC (kulia) akijaribu kumzuia Ribera Inyanje wa Carolina for Kibera kwenye nusu fainali ya wasichana kuwania ubingwa wa Mkoa wa Nairobi katika shindano la Chapa Dimba na Safaricom Season Two Uwanjani Goan Institute Nairobi. Carolina for Kibera ilishinda kwa magoli 4-3 kupitia mipigo ya matuta. Picha/ John Kimwere

Wasichana wa Carolina for Kibera walifuzu kushiriki fainali walipokomoa Dagoretti Mixed kwa mabao 4-3 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare tasa.

Nao wachezaji wa Acakoro Ladies waliokosa tiketi ya fainali za kitaifa mwaka uliyopita walipozabwa na Beijing Raiders, walichoma County Queens kwa magoli 4-1 katika patashika iliyoshuhudia msisimko wa kufa mtu.

Acakoro Ladies ilivuna ufanisi huo kupitia Sylvia Makhungu aliyepiga mbili safi, huku Florence Achieng na Catherine Awuor kila mmoja akifunga bao moja. Bao la kufuta machozi la County Queens lilifumwa na Millicent Lukoje.

”Tumejaa furaha tele kujikatia tiketi ya fainali za Mkoa wa Nairobi ingawa haikuwa mteremko. Tuna imani baadhi ya wachezaji wetu watateuliwa katika timu ya taifa itakayokwenda nchini Uhispania,” kocha wa Carolina for Kibera, Fredrick Odhiambo alisema.

Kando na tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za kitaifa timu itakayoibuka bingwa (wavulana na wasichana) itatuzwa kitita cha Sh200,000 kila moja huku kila mchezaji akipokea simu ya dhamani ya Sh10,000. Fainali za kitaifa msimu huu zitaandaliwa mwezi Juni mwaka huu katika uwanja wa Kinoru Stadium, mjini Meru.

Washindi watajiunga na mabingwa Mikoa mingine ikiwamo: Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa), wavulana wa Berlin (Kaskazini Mashariki) bila kusahau Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati).

Mabingwa wa kitaifa timu ya wavulana pia wasichana kila moja itatuzwa kitita cha Sh 1 milioni.