Jesus kutochezea Manchester City kwa wiki tatu akiuguza jeraha la mguu
Na MASHIRIKA
MSHAMBULIAJI Gabriel Jesus wa Manchester City atasalia nje kwa majuma matatu kuuguza jeraha la mguu alilolipata katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Wolves uwanjani Molineux mnamo Septemba 21, 2020.
Shirikisho la Soka la Brazil limethibitisha kwamba Jesus, 23, ameondolewa kwenye kikosi cha Brazil kilichotazamiwa kuvaana na Bolivia na Peru kwenye mechi zijazo za kufuzu kwa Copa America 2021.
Licha ya kupata jeraha katika dakika ya 66 wakati akichezea Man-City dhidi ya Wolves, Jesus alisalia uwanjani kwa kipindi kizima cha dakika 90 na akafunga bao katika ushindi wa 3-1 waliouvuna.
Kuumia kwa Jesus ni pigo kubwa kwa Man-City ambao pia watakosa huduma za mshambuliaji Sergio Aguero kwa kipindi cha majuma ssaba yajayo kwa sababu ya jeraha la goti.
“Man-City waliwasiliana na daktari wa timu ya taifa ya Brazil, Rodrigo Lasmar, na kumfahamisha kuhusu ukubwa wa kiwango cha jeraha linalouguzwa na Jesus,” ikasema sehemu ya taarifa ya Shirikisho la Soka la Brazil (CBF).
Brazil watavaana na Bolivia mnamo Oktoba 9, 2020, kabla ya kushuka dimbani kupepetana na Peru mnamo Oktoba 13, 2020.
Man-City watakuwa kesho wenyeji wa Leicester City katika gozi la EPL litakalosakatiwa ugani Etihad.
Vikosi vyote vitajibwaga uwanjani vikijivunia mwanzo bora katika kampeni za EPL msimu huu wa 2020-21.
Man-City ya kocha Pep Guardiola iliwapokeza Wolves kichapo cha 3-1 katika mechi ya kwanza ya msimu huu huku Leicester ya mkufunzi Brendan Rodgers ikiwapepeta Burnley 4-2 ugani King Power.
Mchuano huo ulikuwa wa pili kwa Leicester ambao walitawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16 kusakata ligini hadi sasa baada ya kucharaza limbukeni West Bromwich Albion 3-0 katika mchuano wa ufunguzi wa muhula mnamo Septemba 13.
Ushindi uliosajiliwa na Man-City dhidi ya Wolves ambao waliwabwaga kwenye mikondo miwili ya EPL msimu uliopita wa 2019-20 unatazamiwa kuwapa masogora wa Guardiola motisha zaidi dhidi ya Leicester.
Ari zaidi ya Man-City inatarajiwa kuchangiwa na rekodi nzuri ambayo imewashuhudia wakiibuka na ushindi katika mechi 10 na kuambulia sare mara moja katika jumla ya michuano 11 iliyopita ugani Etihad.
Kati ya mechi hizo zote, Man-City wamewafunga wapinzani wao jumla ya mabao 26-1 kutokana na saba zilizopita.
Tangu 1989-90, Man-City hawajapoteza shindano lolote la mwanzo wa msimu uwanjani Etihad. Hiyo ni rekodi waliyoiendeleza mnamo Septemba 24, 2020 kwa kuwabandua Bournemouth kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup kwa kichapo cha 2-1.
Ndoto za Leicester kwenye Carabao Cup hata hivyo yalizimwa ghafla na Arsenal waliowachabanga 2-0 uwanjani King Power na kujikatia tiketi ya kuchuana na Liverpool kwenye hatua ya 16-bora.
Iwapo watajinyanyua na kuwaangusha Man-City, basi ushindi wa Leicester utakuwa wa tatu mfululizo kwenye mechi tatu za kwanza za EPL tangu 1922-23.
Liam Delap, 17, aliyeridhisha dhidi ya Bournemouth atachezeshwa ligini kwa mara ya kwanza. Kukosekana kwa Jesus na Aguero kutampa chipukizi huyo raia wa Uingereza fursa ya kushirikiana na Raheem Sterling na Phil Foden kwenye safu ya mbele ya Man-City.