Michezo

Jezi nambari 7 sasa yapewa Saka

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

CHIPUKIZI Bukayo Saka amepokezwa jezi nambari saba mgongoni kambini mwa Arsenal.

Hata hivyo, kinda huyo mzawa wa Uingereza atavalia jezi yake nambari 77 mgongoni katika mchuano wa mwisho wa mwisho wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu dhidi ya Watford mnamo Julai 26 kisha katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea mnamo Agosti 1, 2020 uwanjani Wembley, Uingereza.

Tangu aanze kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal, Saka ambaye alitia saini mkataba mpya uwanjani Emirates mwanzoni mwa Julai 2020, ametia fora mno na juhudi zake zimetambuliwa na usimamizi wa kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mikel Arteta.

Jezi nambari saba kambini mwa Arsenal ilisalia bila mmiliki tangu kuondoka kwa kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Armenia, Henrikh Mkhitaryan aliyejiunga na AS Roma mwishoni mwa muhula uliopita wa 2018-19. Masogora wengine wa haiba kubwa ambao waliwahi kuvalia jezi nambari saba kambini mwa Arsenal ni Alexis Sanchez, Tomas Rosicky, Robert Pires, Ray Parlour na Paul Merson.

Kati ya mabadiliko mengine ambayo yamefanywa na Arsenal kadri wanavyojizatiti kwa kampeni za msimu ujao ni yale yatakayomshuhudia beki William Saliba akivalia jezi nambari nne mgongoni.

Mfaransa huyo alisajiliwa na Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita wa 2018-19 kutoka St Etienne kwa kima cha Sh3.8 bilioni na akasalia kukiwajibikia kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Jezi nambari nne kambini mwa Arsenal imekuwa ikivaliwa na kiungo mzawa wa Misri, Mohamed Elneny, 28, ambaye kwa sasa anachezea Besiktas ya Uturuki kwa mkopo. Elneny anayetazamiwa kurejea uwanjani Emirates kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21, sasa atavalia jezi nambari 25.