Michezo

Jezi zote EPL kuandikwa #BlackLivesMatter

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MAJINA ya wachezaji nyuma ya jezi zao zitabadilishwa na maandishi ‘Black Lives Matter’ (yaani maisha ya watu weusi ni muhimu) katika jumla ya mechi 12 za kwanza za kurejelewa kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kipute cha EPL kinatarajiwa kuanza upya mnamo Juni 17, 2020 kwa mechi mbili zitakazokutanisha Aston Villa na Sheffield United ugani Villa Park kisha Manchester City na Arsenal uwanjani Etihad.

Mechi hizo ni zile zilizokuwa zimesalia kwa vikosi hivyo kusakata ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo wapinzani wote wengine 16 walikuwa wamepiga hadi kipute hicho kiliposimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mwanzoni mwa Machi 2020.

Mechi zote za raundi nzima ya 30 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Ijumaa ya Juni 19 na Jumapili ya Juni 21, 2020.

Wanasoka wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) tayari wamesimama pamoja na raia wa Amerika na wengine wote ambao wamekuwa wakiandamana kulalamikia ubaguzi wa rangi kufuatia tukio la polisi kumuua  Mmarekani mweusi, George Floyd.

“Sisi wachezaji tunasimama pamoja kwa lengo moja la kuangaamiza ubaguzi wa rangi katika mataifa yote duniani. Tumejitolea kuhakikisha kwamba tunashuhudia jamii ya itakayomkumbatia kila mtu popote atakapokuwa dunia, jamii itakayoheshimu haki za kila mmoja na kutoa nafasi sawa kwa kila mmoja bila kujali jinsia, rangi au misingi ya dini zao” ikasema sehemu ya taarifa ya vikosi vya EPL.

Nembo mpya yenye maandishi ‘Black Lives Matter’ na nyingine itakayokuwa na ujumbe wa shukran kwa maafisa wa afya nchini Uingereza kwa juhudi zao za kukabiliana na virusi vya corona, zitadumishwa kwenye jezi za wachezaji wote wa EPL hadi kampeni za msimu huu zitakapotamatika rasmi.

Baadhi ya wachezaji wa vikosi vya EPL tayari wamekuwa ‘wakipiga goti moja chini’ mazoezini na kusambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii kama ishara ya kupinga ubaguzi wa rangi. Isitoshe, shirika la kijamii la ‘Kick It Out’ nchini Uingereza limekuwa likiwasisitizia wanasoka wa EPL kuendelea kufanya hivyo kila wanapokuwa uwanjani.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) limewataka wachezaji ‘kutumia akili na kuchunguza mambo’ wanaposhiriki maandamano ya aina hiyo.

Kufikia sasa, wanachezaji wanne akiwemo chipukizi wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Uingereza, Jadon Sancho, walichunguzwa na vinara wa soka ya Ujerumani kwa kujitokea hadharani kupinga tukio la ubaguzi la rangi lililochangia kifo cha Floyd, 46, nchini Amerika mwezi uliopita. Wanne hao hawakupokezwa adhabu yoyote.