JICHO KWA FA: Guardiola awataka Manchester City walinyanyue pia Kombe la FA
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
BAADA ya kuwaongoza wachezaji wake kunyanyua ubingwa wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wikendi jana, kocha Pep Guardiola amefichua maazimio yake mengine ya msimu huu.
Kwa mujibu wa kocha huyo mzawa wa Uhispania, kikosi chake kina kiu ya kutia kapuni ufalme wa Kombe la FA na hivyo kufikisha jumla ya mataji matatu kibindoni mwao mwishoni mwa msimu huu.
Man-City wameratibiwa kuchuana na Watford katika fainali ya Kombe la FA itakayowakutanisha uwanjani Wembley mnamo Mei 18. Mbali na kufukuzia Kombe la FA na kutwaa ufalme wa EPL, Man-City walitawazwa mabingwa wa Carabao Cup mnamo Februari baada ya kuwazidi nguvu Chelsea kwenye fainali.
Tija ya kuhifhadhi ubingwa wa Kombe la FA ni ufanisi uliowajia Man-City miaka 10 baada ya Manchester United kuwa kikosi cha kwanza kuweka historia ya kutetea ufalme wa taji la EPL kwa misimu miwili mfululizo.
Baada ya Glenn Murray kuwafungia Brighton bao lililowaweka kifua mbele dhidi ya Man-City kunako dakika ya 27 jijini Sussex, wingu la matumaini lilitanda uwanjani Anfield walikokuwa wakichezea Liverpool na Wolves.
City kujikwaa
Kujikwaa kwa Man-City ama kwa kulazimishiwa sare au kupepetwa na Brighton kungaliwazolea Liverpool ubingwa wa taji la EPL baada ya kuwachabanga Wolves.
Ingalikuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kutia kapuni taji hilo baada ya miaka 29.
Sergio Aguero aliwaongoza Man-City kutoka nyuma na kusajili ushindi wao wa 14 mfululizo katika ligi. Kwa ujumla, Man-City walijivunia ushindi kutokana na mechi 32 kati ya 38 msimu huu na hivyo kuifikia rekodi walioiweka katika kampeni za muhula uliopita.
Mabao mengine ya Man-City katika ushindi huo wa 4-1 uwanjani American Express Community, yalifumwa wavuni kupitia kwa Aymeric Laporte, Riyad Mahrez na Ilkay Gundogan.
Ingawa Man-City hawakufikia rekodi ya alama 100 walioiweka msimu jana, walijivunia mojawapo ya misimu ya kuridhisha zaidi katika kivumbi cha EPL hasa ikizingatiwa ushindani mkali waliolazimika kukabiliana nao kutoka kwa Liverpool.
Licha ya kuwapokeza Wolves kichapo cha 2-0 ugani Anfield, Liverpool walishindwa kukomesha ukame wa miaka 29 wa Kombe la EPL kabatini mwao.
Ilivyo, masogora hao wa kocha Jurgen Klopp waliongoza jedwali kwa dakika 21 za kipindi cha kwanza kabla ya ushindi wa Man-City kuwapiga kumbo hadi nafasi ya pili.
Liverpool ambao walipoteza mchuano mmoja pekee, kusajili ushindi mara 30 na kuambulia sare mara saba, walikamilisha kampeni za EPL kwa alama 97, moja pekee nyuma ya Man-City.
Mabao ya Liverpool yalijazwa kimiani na mvamizi Sadio Mane ambaye kwa pamoja na Mohamed Salah wa Liverpool na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal, walitawazwa wafungaji bora wa msimu baada ya kujivunia mabao 22 kila mmoja.
Alisson Becker wa Liverpool alitawazwa Kipa Bora wa msimu baada ya wapinzani kushindwa kumfunga bao katika jumla ya mechi 21.
Alama 97 zilizovunwa na Liverpool katika kampeni za msimu huu zinakuwa za tatu kwa wingi zaidi baada ya 98 za Man-City na pointi 100 zilizorekodiwa na wafalme hao mnamo 2017-18.