• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Jinamizi la pufya latesa Kenya inayojizatiti kwa Riadha za Dunia Qatar

Jinamizi la pufya latesa Kenya inayojizatiti kwa Riadha za Dunia Qatar

Na GEOFFREY ANENE

SIKU chache kabla ya Riadha za Dunia kuanza hapo Septemba 27 jijini Doha nchini Qatar, Kenya inakabiliwa na tishio la kupigwa marufuku na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) baada ya runinga moja nchini Ujerumani kufichua uozo zaidi wa matumizi ya dawa za kusisimua misuli (pufya) miongoni mwa wanariadha wa Kenya.

Mkuu wa Kitengo cha Maadili ya Riadha kwenye shirikisho hilo (AIU), Brett Clothier alisema kuwa Kenya huenda ikachukuliwa hatua hiyo baada ya kupokea ushahidi kutoka kwa runinga ya ZDF yenye makao yake mjini Mainz kuwa wanariadha wengi wa Kenya wanatumia dawa aina ya EPO kujiongeza nguvu.

“Haya ni madai mabaya sana na sisi si watu wasiojua kuwa matatizo kama hayo pamoja na ufisadi hupatikana Kenya. Sisi huwa tayari kupokea ushahidi na kujaribu kuchunguza madai ya visa hivi,” Clothier alinukuliwa na runinga hiyo akisema kabla ya kuongeza, “Kuna mataifa matano tuliyotiwa katika kategoria ya A. Katika mataifa haya, wanariadha wanatumia sana dawa za kusisimua misuli na kwa hivyo tumeyawekea sheria kali yanazostahili kufuata. Kenya ni moja ya mataifa hayo na unapokosa kufuata sheria hizi, basi Shirikisho la Riadha Duniani linaweza kukupiga marufuku.”

Katika ufichuzi wake, runinga hiyo inadai kuwa wanariadha wawili walio katika timu ya Kenya inayojiandaa kuelekea Doha wametibiwa na dawa ya EPO.

“Mwanariadha mmoja mwanamume na mwingine mwanamke walinaswa kwenye video kwa kutumia kamera zilizofichwa wakidungwa sindano ya dawa ya EPO moja kwa moja kwenye mishipa yao,” runinga hiyo ilisema Jumapili.Iliongeza kuwa ilizungumza na daktari mmoja ambaye hakutaka kutajwa aliyedai kuwa alikuwa na wanariadha wanane katika timu ya taifa ya sasa.

Shirikisho la Riadha nchini (AK), runinga ya ZDF ilisema, lilizungumzia ufichuzi huo. Lilinukuu mmoja wa maafisa wa AK, Barnabas Korir, akisema, “Tunahakikisha kuwa timu yetu ya taifa inafuata sheria. Tulizungumza sana na timu hii, tukaiandalia warsha na kuieleza sheria zote za kimataifa na pia kupima wanariadha mara kadhaa. Wanariadha wanajua adhabu ya kutumia dawa za kusisimua misuli ni kutupwa nje ya timu na kupigwa marufuku kabisa kuwakilisha Kenya.”

Madai makali

Runinga hiyo ilitoa madai mengine makali kuwa huenda kiini cha kuenea kwa uovu huu ni ufisadi mkubwa kati ya AK na Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na matumizi ya pufya la Kenya (ADAK).

Mmoja wa wafanyakazi wa zamani wa ADAK alieleza ZDF, “Wanaficha matokeo ya wanariadha kadhaa ili mwanariadha asipigwe marufuku. AK na ADAK zinafanya kazi pamoja na kupata mapato kwa kufanya hivyo. Wanariadha ama mameneja wao lazima walipie huduma hiyo.”

Runinga hiyo pia imedai kuwa ina stakabadhi rasmi kutoka kwa Shirikisho la Riadha nchini zinazoonyesha kuwa mfanyakazi wake mmoja wa ngazi ya juu aliandikia barua meneja mmoja mtajika wa riadha akisema, “Uchunguzi wa pufya wa kwanza (A) na wa pili (B) unaonyesha mwanariadha alitumia dawa za kusisimua misuli. Tafadhali tukutane haraka iwezekanavyo kujadiliana haya.”

Mwaka 2015 na 2016, Kenya iliponea tundu la sindano kukosa michezo ya Olimpiki na mashindano mengine kutokana na uovu huu.

  • Tags

You can share this post!

TEKNOLOJIA: Wanafunzi wako tayari, nani atawafundisha...

USIU-A yapata matokeo mseto katika ligi ya hoki

adminleo