Jinsi Arsenal waliitoa Liverpool pumzi
ARSENAL walidhihirisha kuwa wangali na fursa na uwezo wa kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kutandika Liverpool 3-1 katika kipute hicho ugani Emirates, Jumapili.
Matokeo hayo yaliacha Arsenal na alama 49, mbili pekee nyuma ya Liverpool wanaoselelea kileleni mwa jedwali la EPL baada ya kutandaza pia mechi 23.
Arsenal sasa wameshinda mechi tatu mfululizo tangu Januari 7 walipokubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa Liverpool wakiwadengua kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA.
Ushindi kwa Liverpool ungedidimiza pakubwa matumaini ya Arsenal kuendeleza presha kwa washindani wao wakuu ligini muhula huu, ikiwemo mabingwa watetezi Manchester City.
Hadi waliposhuka dimbani kuvaana na Arsenal, Liverpool walikuwa wamepoteza mechi moja pekee ligini msimu huu.
Hiyo ilikuwa dhidi ya Tottenham Hotspur waliowakomoa 2-1 mnamo Septemba 2023.
Inter yaselelea Serie A
Nchini Italia, Inter Milan ilifungua pengo la pointi nne kileleni mwa Ligi Kuu (Serie A) baada ya kufinya Juventus 1-0 ugani San Siro.
Bao la pekee katika pambano hilo lilifumwa wavuni na Federico Gatti aliyejifunga.
Inter sasa wanajivunia alama 57, nane zaidi kuliko nambari tatu AC Milan.
Miamba hao walinyanyua taji la Serie A mara ya mwisho mnamo 2020-21 na watavaana na AS Roma ugenini katika mchuano wao ujao wikendi hii.
Juventus wanakamata nafasi ya pili kwa alama 53 huku pengo la pointi 14 likiwatenganisha na nambari nne Atalanta waliocharaza Lazio 3-1.
Real Madrid watupa alama La Liga
Kule Uhispania, Atletico walifunga bao katika dakika ya mwisho na kulazimishia Real Madrid sare ya 1-1 katika Ligi Kuu (La Liga).
Goli lilifumwa wavuni na Marcos Llorente aliyefuta juhudi za Brahim Diaz ugani Bernabeu.
Atletico sasa wanafunga mduara wa nne-bora jedwalini kwa alama 48, mbili nyuma ya mabingwa watetezi Barcelona.
Girona ni wa pili kwa pointi 56, mbili nyuma ya Real wanaoselelea kileleni baada ya mechi 23.