Michezo

Jinsi Tanzania imejipanga AFCON mara hii kuepuka fedheha ya 2019 iliposhika mkia kundini

January 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI 

MWAKILISHI wa kipekee wa Afrika Mashariki katika dimba la Klabu bora barani Afrika (Afcon) 2023 ni Tanzania na timu yake ya Taifa Stars chini ya ukufunzi wa Adel Amrouche kutoka nchi ya Algeria.

Tanzania imeshiriki michuano hiyo ambayo inaingia awamu ya 34 nchini Ivory Coast kati ya Januari 13 hadi Februari 11 mara mbili, 1980 na 2019.

Katika mara hizo mbili, ilitolewa katika awamu ya makundi, kwa ujumla ikipata pointi 1 kati ya zote 18 kwa kufunga mabao 5 huku nayo ikifungwa mara 14.

Hii ina maana kwamba taifa hilo linashiriki makala hayo kwa mara ya tatu sasa na pia limejihakikishia kushiriki mwaka wa 2027 kama mwenyeji wa dimba hilo pamoja na majirani; Kenya na Uganda.

Katika awamu ya 12 ya makala hayo nchini Misri, Tanzania ilipoteza michuano miwili huku ikitoka sare mara moja na taifa la Ivory Coast.

Taifa Stars ilikuwa imepangwa katika kundi A pamoja na Nigeria, Misri na Ivory Coast.

Nigeria iliadhibu Tanzania kwa magoli 3 kwa 1, Misiri ikawakanya kwa 2-1 na kumalizia na sare ya 1-1 na Ivory Coast.

Kijumla, ilizoa pointi 1 ikiwa ya mwisho katika kundi hilo ikiwa imetikisa nyavu za wapinzani mara tatu lakini zao zikitikiswa mara 6.

Mwaka wa 2019 Tanzania ilijipata katika kundi moja na Kenya, Algeria na Senegal ambapo tena iliibuka ya mwisho katika kundi hilo la C.

Tanzania ilipepetwa kwa magoli 3-2 na majirani wao Kenya, hali ambayo ilifanya imfute kocha wao Emmanuel Amunike.

Dimba hilo la awamu ya 34 likishirikisha mechi 52 litahusisha timu 24, Tanzania ikiwa katika kundi la F pamoja na Morocco, DR Congo na Zambia.

Kando na Tanzania, mataifa mengine katika dimba hilo ni wenyeji Ivory Coast, Nigeria, Equatorial Guinea, na Guinea-Bissau katika kundi A huku kundi B likijumuisha Misiri, Ghana, Cape Verde na Mozambique.

Kundi la C lina Senegal, Cameroon, Guinea na Gambia huku kundi D likiwaleta pamoja Algeria, Burkina Faso, Mauritania na Angola huku kundi E likiwa na Tunisia, Mali, Afrika Kusini na Namibia.

Mechi hizo zitaandaliwa katika nyuga za jiji kuu Abidjan, ndizo Felix Houphouet-Boigny na Alassane Ouattara Stadium.

Zingine ni Yamoussoukro, Bouake, Korhogo na San Pedro.

Kwa sasa, kombe hilo limeshikiliwa na Senegal.

Misri ndiyo imeshinda kombe hilo kwa mara nyingi zaidi, saba, Cameroon ikifuata kwa mara tano, Ghana, nne na DRC na Ivory Coast mara mbili kila mmoja.

 

[email protected]