Joe Hart kuondoka Burnley Julai
Na CHRIS ADUNGO BURNLEY wamethibitisha kwamba hawatarefusha zaidi mkataba wa kipa wa zamani wa Uingereza, Joe Hart, baada ya Juni 30, 2020. Hart, 33, alijiunga na Burnley almaarufu ‘The Clarets’ mnamo 2018 baada ya kukatiza uhusiano wake na Manchester City kwa kima cha Sh490 milioni. Tangu Burnley wapokezwe kichapo cha 5-1 kutoka kwa Everton mnamo Disemba 2019, Hart alipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza na amewajibishwa mara tatu pekee katika mapambano ya League Cup. Nick Pope ndiye kipa chaguo la kwanza la Burnley kwa sasa huku nambari pili akiwa Bailey Peacock-Farrell, 23, ambaye ni mzawa wa Ireland Kaskazini. Chipukizi huyo hajawajibishwa na Burnley katika mchuano wowote wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi kufikia sasa msimu huu. Taaluma ya Hart iliporomoka ghafla tangu awe sehemu muhimu ya kikosi cha Man-City kilichonyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya EPL mnamo 2012 na 2014. Katika misimu hiyo, Hart ambaye pia amechezea timu ya taifa ya Uingereza mara 75, alitawazwa Kipa Bora wa Mwaka. Kubanduka kwake kambini mwa Man-City kulichochewa zaidi na uhusiano mbaya uliotamalaki kati yake na kocha Pep Gaurdiola ambaye kwa sasa ameapa kuwanyanyulia Man-City ufalme wa EPL na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao kabla ya kuondoka rasmi uwanjani Etihad. Hadi alipoingia katika sajili rasmi ya Burnley, Hart aliwahi pia kuwadakia Torino na West Ham United kwa mkopo kutoka Man-City. |