Joe na Edward watetemesha Super 8
Na JOHN KIMWERE
WANASOKA Joe Abong’o na Edward Peter kila mmoja alipiga kombora moja safi kwenye mechi za Super Eight Premier League (S8PL) na kubeba Githurai Allstars na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) kuzoa alama tatu muhimu.
Githurai Allstars na TUK kila moja ilijiongezea ufanisi huo baada ya kufunika kimiani bao 1-0 dhidi ya Lebanon FC na Mathare Flames mtawalia.
Nao mabingwa watetezi, Jericho Allstars ambayo hunolewa na kocha, Thomas Okongo ilionyesha kivumbi kikali na kukubali kulala kwa magoli 2-0 mbele ya majirani zao Madakara J.L.S.A kwenye patashika iliyopigiwa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.
”Kusema kweli nawapawa hongera wachezaji wangu wanaendelea kukazana kwa udi na uvumba kukabili wapinzani wetu kwenye mechi za muhula huu,” alisema kocha wa Githurai Allstars, Geoffrey Onyango na kuongeza kuwa wamepania kuendeleza mtindo huo ili kutimiza azimio lao.
Kwa upande wa TUK, kocha wake, Luke Aluoch alisema “Ingawa tumejikuta pambaya mbele ya wapinzani wetu nashukuru kikosi changu kwa jumla kinaendelea kuonyesha dalili za kuzinduka.”
Wachana nyavu wa Makadara J.L.S.A wanaoketi katika mduara hatari wa kuteremshwa daraja walifanya kweli kuangusha wanzao hao kupitia juhudi Kaycy Odhiambo na Erickson Kamweru walipocheka na nyavu mara moja kila mmoja.
Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, NYSA ya kocha, Fredrick ‘Oti’ Otieno iliangukia pua iliponyukwa mabao 2-0 na MASA, nacho kikosi cha Meltah Kabiria kinaokuja kwa kasi msimu huu kilichomokla na ushindi wa magoli 3-2 mbele ya Huruma Kona.
Nayo Rongai Allstars ilishindwa kufana na kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 Shauri Sportiff.
MATOKEO YA WIKENDI
Mathare Flames 0-1 TUK
Madakara J.L.S.A 2-0 Jericho Allstars
MASA 2-0 NYSA
Meltah Kabiria 3-2 Huruma Kona
Githurai Allstars 1-0 Lebanon FC
Rongai Allstars 1-1 Shaurimoyo Sportif FC