John Waw sasa kuwanoa makipa wa Sofapaka
Na CHRIS ADUNGO
SOFAPAKA wameendelea kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 katika Ligi Kuu kwa kujinasia huduma za kocha wa makipa John Waw kutoka Soy United inayoshiriki Ligi ya Daraja la Pili.
Hadi alipoangika glavu zake, Waw ambaye ametia saini mkataba wa mwaka mmoja na Sofapaka, alikuwa mwanasoka wa kikosi cha Chemelil Sugar katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
“Sasa nimeagana rasmi na Soy United na nimeingia katika sajili ya Sofapaka kwa kandarasi ya mwaka mmoja. Hii ni hatua kubwa kwangu kitaaluma,” akasema Waw.
“Najua kwamba matarajio sasa ni makubwa zaidi. Lakini nitajitahidi kusaidia Sofapaka kutimiza mengi ya malengo yao ya msimu ujao chini ya mkufunzi John Baraza,” akaongeza.
Sofapaka, ambao waliibuka mabingwa wa KPL mnamo 2009, wamejishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji na tayari wamejinasia huduma za wanasoka Michael Bodo (Kariobangi Sharks), Roy Okal (Mathare United) kipa Kevin Omondi na fowadi Paul Kiongera (Wazito FC).
Kati ya wanasoka wa mataifa ya nje ambao wamesajiliwa na Sofapaka ni mshambuliaji Michael Tuborlayefa Karamor aliyebanduka kambini mwa Lagos Athletico ya Nigeria na beki Isaac Mitima aliyesajiliwa kutoka APR ya Rwanda.
Kwa mujibu wa Elly Kalekwa ambaye ni rais wa Sofapaka, kikosi chake kina kiu ya kujizolea taji la KPL kwa 2009.
“Tunasuka kikosi kitakachohimili ushindani mkali ligini. Kubwa zaidi katika maazimio yetu ni kunyanyua taji la msimu ujao. Hiyo ndiyo sababu ambayo imetuchochea kuwaendea wanasoka wa haiba kubwa watakaotusaidia kutimiza hayo,” akasema kwa kufichua kwamba wako pua na mdomo kumsajili kiungo Lawrence Juma wa Gor Mahia.
“Tupo katika hatua za mwisho za kurasimisha uhamisho wa Juma kutoka Gor Mahia. Ni mwanasoka wa haiba kubwa ambaye ataleta mwamko mpya kikosini.”
Katika kampeni za msimu uliopita, Sofapaka almaarufu ‘Batoto ba Mungu’ waliambulia nafasi ya 10 baada ya kujizolea jumla ya alama 31 kutokana na mechi 23.
Chini ya kocha Baraza ambaye ni fowadi wa zamani wa Harambee Stars, Sofapaka walisajili ushindi mara nane, kuambulia sare mara saba na kupoteza mechi nane za KPL mnamo 2019-20.