• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Juja Farm yapiga moyo konde kujiimarisha uwanjani

Juja Farm yapiga moyo konde kujiimarisha uwanjani

Na LAWRENCE ONGARO

ILI kutimiza matamanio ya kuinua soka mashinani hadi ngazi ya kitaifa, panahitajika wachezaji chipukizi kunoa makali yao, anasema kocha wa kikosi cha Juja Farm Bw Patrick Kamau.

Kwa muda mrefu kikosi cha Juja Farm kimekuwa mwiba mkali katika mashinani huku ikitesa timu nyingi katika eneo hili.

Kocha huyo anasema kuwa lengo lake kuu ni kuona ya kwamba vijana hawa wanasonga katika kiwango kingine muhimu cha soka kwani wanayo bidii kama ya mchwa.

Mazoezi yao hufanywa katika uwanja wa shule ya Juja Farm Primary kati ya Jumatatu hadi Ijumaa ili wajiandae kwa mechi za kirafiki ifikapo mwishoni mwa wiki.

“Kwa wakati huu timu hii inategemea mechi za kujipima nguvu na zile za mataji huku wakijioandaa kwa Ligi ya kaunti ndogo ya Thika ifikapo msimu ujao wa 2020,” alisema Kamau.

Alisema kwa wakati huu wanashiriki katika mechi ya kuwania taji la Kalimoni Youth Cup lakini walibanduliwa katika nusu fainali na Ndarugu FC baada ya kutingwa mabao 3-1 na Ndarugu FC. Hata hivyo kabla ya kuzimwa katika mechi hiyo waliweza kuilaza Gachororo mabao 2-1. katika mechi nyingine waliichapa Premier Bag kwa bao 1-0.

Katika mechi za kirafiki walizocheza hivi majuzi vijana hao waliichapa Webbs FC ya Thika kwa bao 1-0. Juja Farm iliweza kuilaza Kiaora Stars kwa mabao 2-0. Halafu walitoka sare na Muchatha kwa kulimana bao 1-1.

Licha ya kuwanoa katika mchezo wa soka pia nina wapa mawaidha kuhusu ubaya wa kutumia dawa za kulevya na kutojihusisha na maovu mabaya.

“Kwa wakati huu pia ninatafuta usaidizi kutoka kwa wafadhili ambao wangeweza kutupiga jeki ili ifikapo msimu ujao tuweze kujiweka tayari kujiendeleza katika kiwango kingine cha juu,” alisema Kamau.

Anatoa mwito kwa wakazi wa Juja Farm wamuunge mkono ili aweze kufanya mengi  kwa kuwainua vijana hao.

Anazidi kueleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa klabu hicho miaka minne iliyopita wamepitia panda shuka nyingi lakini changa moto hizo wameweza kuzikabili vilivyo.

Anasema kuwa na dhamira ya kunoa timu hiyo hadi ifaulu kuibua wanasoka mahiri wenye uwezo wa kujiunga na timu za taifa katika siku zijazo.

You can share this post!

‘Punguza Mizigo’ yagawanya wanasiasa

Vitimbi vya ‘Kamata Kamata’ vyarudi Rotich akibambwa

adminleo