Juma arejea nyumbani baada ya kutimuliwa Afrika Kusini
NA CECIL ODONGO
MSHAMBULIZI wa Harambee Stars Masoud Juma amerejea nchini baada ya kukatiza kandarasi yake ya miezi minane na klabu ya Cape Town City inayoshiriki ligi kuu ya Absa nchini Afrika Kusini.
Juma alikuwa miongoni mwa wachezaji kutoka nchi za kigeni waliokuwa wakikodolewa macho na shoka la kutimuliwa baada ya timu hiyo kumsajili kipa Peter Leeuwenburgh kutok Ajax Amsterdam ya Uholanzi ,iliyofikisha idadi ya wachezaji hao hadi sita ingawa sheria inasema hawafai kuzidi watano.
Mwanadimba huyo wa zamani wa Kariobangi Sharks hajapata timu ya kusakatia japo kwa sasa anapumzika na kutangamana na famila, jamaa na marafiki. Yeye hutumia muda wake mwingi kupigana dhidi ya matumizi ya mihadarati katika mji wake wa nyumbani wa Isiolo.
Vile vile straika huyo anapanga kuanzisha mashindano yatakayohusisha timu 16 kama njia ya kutoa hamasisho dhidi ya matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana wa eneo hilo.
“Tatizo la matumizi ya mihadarati limekuwa dondasugu hapa nyumbani na nimekuwa nikilifuatilia sana kwenye mitandao ya kijamii. Kwa sababu sasa nipo nyumbani lazima nipigane nalo na kuwaokoa vijana wengi waliona uraibu wa kutumia dawa hizo,” akasema Juma.
Aidha alisisitiza kwamba mashindano hayo yatakuwa ya manufaa makubwa kwa wanafunzi wa shule za msingi, shule za upili, vyuo anuwai na vyuo vikuu wakati huu wapo likizoni.
Kulingana na Juma, mashindano hayo yatang’oa nanga Agosti 8 na yakamilike Agosti 22 katika uwanja wa Bula Mpya mjini Isiolo.