Juma ‘Babu’ Abdalla adhibiti mikoba ya Murang’a Seal
Na MWANGI MUIRURI
KOCHA Dennis ‘Wise’ Okoth amethibitisha kujiondoa kutoka timu ya soka ya Murang’a SEAL iliyo na asili yake katika Kaunti ya Murang’a.
Okoth alikuwa akitekeleza majukumu kama kaimu kocha wa timu hiyo ambayo hivi majuzi ilikuwa imezua msisimko katika ligi kuu ya kitaifa (FKF) kabla ya kuanza mteremko bila matuta ya kudhibiti kufifia.
Hii ni baada ya kumtema kocha wao Gabriel ‘Kingi’ Njoroge mwishoni mwa mwaka 2023 kama njia ya kudhibiti mporomoko huo katika jedwali.
Njoroge aliongoza timu hiyo kujibwaga ugani mara 16 hadi mwishoni mwaka 2023 matokeo yakiwa ni ushindi mara sita, sare mara nne na kupoteza mara tano.
Okoth pia alikuwa ndiye naibu kocha na kwa sasa akikabidhi mikoba yake kwa kocha mpya Juma ‘Babu’ Abdalla, amemtahadharisha kwamba “hakuna lifti za kufika kileleni mwa soka, hali ni kukwea tu”.
Kwa sasa, M-Seal ikiwa na pointi 24 inashikilia nafasi ya 10 katika jedwali linaloongozwa na Gor Mahia ikiwa na pointi 40 baada ya mechi 18.
Msimu ukianza M-Seal ambao asili yao ni walinzi wa G4S ambao walikuja pamoja na kuunda timu hiyo chini ya udhamini wa mwekezaji wa kaunti hiyo Bw Robert Macharia, ilikuwa ikibishania nafasi ya kutwaa ligi.
Uwanja wao wa nyumbani ambao ni wa mwekezaji binafsi, unafahamika kama St Sebastian almaarufu ‘Shakahola’.
Uwanja huo uko katika kijiji cha mashinani kabisa ambapo ili kuufikia, ni unatumia barabara ya vumbi inayopitia kwa vichaka.
Kutokana na ‘ushakahola’ wa uga huo, timu hiyo hivi majuzi iliandikia kamati ya kiusalama Murang’a ikiteta kwamba walanguzi na watumizi wa mihadarati walikuwa wameugeuza maskani yao.