Michezo

Junior Starlets yalima Burundi 3-0 kuweka hai matumaini ya kushiriki Kombe la Dunia U-17

June 9th, 2024 2 min read

Na TOTO AREGE

TIMU ya Kenya ya akina dada walio chini ya umri wa miaka 17 Junior Starlets, inanusia kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu, baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Burundi.

Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza wa raundi ya nne ya kuwania tiketi ya kufuzu, ilichezewa katika uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, Ethiopia mnamo Jumapili.

Mechi ya marudiano itachezwa katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, Jumapili ijayo.

Starlets inatarajiwa kutua nchini Jumatatu na kwenda moja kwa moja kambini – katika Hoteli ya Stadion, Nairobi.

Ili kuhakikisha nafasi yao kwenye Kombe la Dunia, Kenya inahitaji sare yoyote, au kuzuia kufungwa zaidi ya magoli matatu wakati watamenyana na Burundi.

Mshambuliaji Lorna Faith alikuwa wa kwanza kutinga wavuni bao katika dakika ya 11 kabla ya kiungo wa kati Marion Serenge kuongeza bao la pili dakika ya 43, ikipatia Kenya uongozi katika kipindi cha kwanza.

Katika kipindi cha pili, Burundi hawakuweza kurudi katika mechi huku kocha wa Starlets Mildred Cheche akileta nguvu mpya Susan Akoth, ambaye alifunga bao la tatu dakika ya 71 na kupatia Kenya pointi zote muhimu ugenini.

Cheche alifanya mabadiliko mawili kwenye kikosi cha kuanzia yakazaa matunda. Alifanya mabadiliko katika mashambulizi na katikati na kudumisha mlinda lango na mabeki.

Mlinda lango Velma Abwire aliendelea kulinda lango, akisaidiwa na mabeki nahodha Elizabeth Ochaka, Christine Adhiambo, Kimberly Akinyi, na Lorine Ilavonga.

Katikati, Rebbeca Odato alicheza kama kiungo wa kati na Serenge kama mshambuliaji.

Katika nguvu ya mashambulizi, washambuliaji Joan Ogola na Valarie Nekesa walikuwa benchi kupisha Quinter Adhiambo na Lorna Faith.

Katika mechi nyingine barani Afrika, Zambia iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Morocco Jumamosi kwenye Uwanja wa Heroes huko Lusaka, Zambia.

Mshambuliaji wa Zambia Namute Chileshe alifunga mabao katika dakika ya 13, 24 na 82. Goli la Morocco lilifungwa na Azraf Kautar kunako dakika ya 37.

Timu tatu-bora kutoka kwenye mechi za kufuzu za eneo la Afrika, zitawakilisha bara hili kwenye Kombe la Dunia ambapo timu 16 kutoka mashirikisho sita zitawania taji.

Mashindano ya Kombe la Dunia yatafanyika katika Jamhuri ya Dominika kuanzia Oktoba 16 hadi Novemba 3, 2024.