• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Junior Starlets yavuna, DRC ikijiondoa mashindanoni

Junior Starlets yavuna, DRC ikijiondoa mashindanoni

NA TOTO AREGE

TIMU ya taifa ya wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 almaarufu Junior Starlets, imefuzu raundi ya tatu ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2024, baada ya wapinzani wao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kujiondoa mashindanoni.

Kenya ilitarajiwa kuondoka nchini Alhamisi kuelekea Kinshasa kucheza mechi hiyo ya kwanza ya mkondo wa pili Jumapili, lakini haikusafiri.

Mechi ya marudiano ilipangwa kuchezwa  mnamo Februari 9, 2024, jijini Nairobi.

Wachezaji waliripoti kambini katika Stadion Hotel mnamo Jumatano wiki hii na wamekuwa wakifanya mazoezi katika uwanja wa Kasarani Annex jijini Nairobi.

Kufikia Jumatatu wiki hii, wachezaji 26 pekee waliripoti kambini kwa mazoezi na wachezaji wanne kutoka Wiyeta Girls hawakuwa wameingia kambini.

Kenya chini ya kocha mpya Mildred Cheche, sasa itakutana na mshindi kati ya Afrika Kusini na Ethiopia.

Katika mechi za kufuzu za hivi karibuni, Djibouti, Senegal, na Liberia pia wamefuzu kwa raundi ya tatu baada ya, Libya, Equatorial Guinea na Mali, mtawalia, kujitoa kwenye mashindano kabla ya raundi ya kwanza.

Kuna raundi nne za kufuzu kwa Kombe la Dunia, na timu tatu pekee zitapata tiketi ya kuwakilisha Afrika kwenye mashindano ya mwisho huko Jamhuri ya Dominika mnamo Oktoba.

DRC kujitoa kwenye mashindano kunakuja siku moja baada ya timu yao ya wanaume ya Les Leopards kufuzu kwa nusu-fainali katika Kombe la Afrika (Afcon 2023) linaloendelea nchini Cote d’Ivoire baada ya kuishinda Guinea 3-1.

Wamefuzu kwa nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2015. DRC inatarajiwa kukabiliana na ama wenyeji Cote d’Ivoire au Mali katika nusu fainali Jumatano ijayo.

Jamhuri ya Dominica imefuzu kwa Kombe la Dunia moja kwa moja kama wenyeji pamoja na New Zealand.

New Zealand walimaliza Kundi B na ushindi wa mechi tatu mfululizo, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 4-1 dhidi ya Fiji na 7-0 dhidi ya Tonga.

Mashindano haya yameona mabingwa mbalimbali wakitokea miaka iliyopita. Uhispania, baada ya kushinda taji mwaka 2018 na 2022, kwa sasa inashikilia hadhi ya bingwa mtetezi.

DPR Korea pia wamejitokeza kwa kushinda mashindano ya kwanza mwaka 2008 na tena mwaka 2016.

Aidha, Korea Kusini na Japan, kila mojawapo, imeshinda mara moja mwaka 2010 na 2014 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Maiti ya kitoto malaika yatupwa karibu na ofisi ya umma

Mwanamume aliyefungwa jela miaka 30 aomba korti impe mkewe...

T L