Juventus wakabwa koo na limbukeni Benevento kwenye Serie A
Na MASHIRIKA
JUVENTUS walisajili sare ya tano katika mechi tisa za hadi kufikia sasa msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kukabwa na limbukeni Benevento mnamo Novemba 28, 2020.
Kocha Andrea Pirlo wa Juventus alimpumzisha mshambuliaji Cristiano Ronaldo katika mchuano huo. Kutokuwepo kwa nyota huyo raia wa Ureno kulimweka Pirlo katika ulazima wa kumtegemea fowadi Alvaro Morata aliyewaweka Juventus kifua mbele katika dakika ya 21.
Hata hivyo, Gaetano Letizia aliwasawazishia Benevento mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Paulo Dybala alipoteza nafasi maridhawa ya kufungia Juventus bao la ushindi katika dakika ya 89, sekunde chache kabla ya Morata kuonyeshwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu.
Juventus ambao wanajivunia kutia kapuni mataji tisa mfululizo ya Serie A kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini baada ya kusajili ushindi mara nne na kuambulia sare mara tano.
Mikoba ya Benevento kwa sasa inadhibitiwa fowadi wa zamani wa Juventus, Filippo Inzaghi.