Michezo

Kabras, KCB na Homeboyz wanyimana pumzi Kenya Cup

November 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za Kabras Sugar, KCB na Homeboyz zilisalia unyo kwa unyo katika nafasi tatu za kwanza kwenye Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) baada ya kila mmoja wao kuandikisha ushindi wa nne mfululizo, wikendi.

Mabingwa wa mwaka 2016 Kabras bado wanaongoza ligi hii ya klabu 12 kwa tofauti ya ukubwa wa ushindi wa mechi zao.

Wanasukari hawa kutoka Kaunti ya Kakamega wana jumla ya alama 20 baada ya kuzaba washikilizi wa rekodi ya mataji mengi Nondescripts 40-15 uwanjani Jamhuri jijini Nairobi.

Wamevuna alama sawa na mabingwa watetezi KCB, ambao pia wamefikisha alama 20 baada ya kujiongezea alama ya bonasi ya tano mfululizo kwa kuzaba Menengai Oilers 43-13 katika uwanja wa kilimo wa Nakuru.

Homeboyz ndio timu ya mwisho ambayo haijapoteza mechi. Inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 18. Imezoa alama mbili za bonasi. “Madeejay” hao walilipua Western Bulls kutoka kaunti ya Kakamega kwa alama 36-17 uwanjani RFUEA.

Wanabenki wa KCB wataalika Homeboyz uwanjani Ruaraka katika mechi yao ijayo mnamo Novemba 23.

Mabadiliko makubwa yameshuhudiwa katika nafasi tisa za mwisho. Mabingwa wa zamani Impala Saracens na Mwamba wameruka juu nafasi moja kila mmoja na kutulia katika nafasi za nne na tano, mtawalia.

Impala ilishangaza Mwamba 26-24 na kuimarisha alama zao kutoka 10 hadi 15.

Mwamba ilipata alama ya bonasi kwa kupoteza pembamba dhidi ya Impala.

Idadi ya alama za Mwamba sasa ni 11. Oilers, ambayo iliingia mechi za raundi ya nne ikikamata nafasi ya nne, sasa inapatikana katika nafasi ya sita kwa alama 11.

Iko nyuma ya Mwamba kwa sababu imefungwa alama nyingi kuliko ilizofunga.

Blak Blad imepaa nafasi tatu na kutua katika nafasi ya saba kwa alama saba.

Wanafunzi hao wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walitumia uwanja wao wa nyumbani vyema walipobwaga Kisumu 31-3 na kujiongezea alama tano muhimu. Nondescripts waliachilia nafasi hiyo ya saba baada ya kupokea kichapo kikali kutoka kwa Kabras.

Mabingwa hawa mara 17, ambao walishinda ligi mara ya mwisho mwaka 1998, wako katika nafasi ya nane kwa alama sita.

Nakuru yaimarika

Nakuru almaarufu Wanyore ndiyo timu iliyoimarika zaidi baada ya mechi za raundi ya nne kusakatwa. Mabingwa hawa wa mwaka 2013 na 2014, ambao walikuwa wanavuta mkia, sasa wanakamata nafasi ya tisa kwa alama sita.

Bulls inafunga mduara wa 10-bora baada ya kuteremka nafasi mbili. Imesalia na alama tano. Inafuatiwa na Kisumu, ambayo pia imeshuka nafasi mbili.

Kisumu ina jumla ya alama nne. Kenya Harlequin, ambayo ilishikilia nafasi ya 11, sasa inavuta mkia kwa alama mbili.

Harlequin inasalia timu pekee ambayo haijaonja ushindi msimu huu wa 2019-2020.