Kahawa Queens yaanza ligi mpya vyema
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Kahawa Queens iliandikisha ushindi wa alama sita muhimu baada ya kushiriki mechi mbili za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu huu.
Nao vipusa wa Mombasa Olympic walibugizwa mabao 6-1 na Sunderland Samba kwenye mechi iliyochezewa uwanja mabao Congo Boys Serani mjini Mombasa.
Kahawa Queens inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza iliicharaza Mukuru Talent Academy mabao 2-0 kisha kuzoa bao 1-0 mbele ya Soccer Queens. Wachana nyavu wa Kahawa Queens ambao hunolewa na kocha, Joseph Wambua walionyesha mchezo safi na kufanikiwa kuvuna alama zote.
Wasichana hao walipata ufanisi huo kupitia Everlyn Juma aliyepiga mbili safi huku Emily Auma akiitingia bao moja.
”Sina budi kushukuru wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliofanya licha ya kwanza ndiyo mwanzo tunafungua kampeni zetu msimu huu maana haikuwa rahisi kucheza mechi mbili ndani ya siku mbili,” kocha wa Kahawa Queens alisema na kuongeza kuwa wanatarajia kuendeleza mtindo huo kwqenye mechi sijazo.
Nao Sylvia Akoth alitikisa wavu mara mbili wakati Irine Aluoch, Jemimah Akinyi, Lorna Nyarinda na faith Kavinya kila mmoja alipiga moja safi na kubeba Sunderland Samba kunyakua alama tatu ugenini.
Kwenye mechi nyingine, Resah Naliaka na Caroline Mwingereza kila mmoja alifunga goli moja na kusaidia Joylove kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Limuru Starlets. Kwenye jedwali, Moving The Goalpost (MTG) ingali kifua mbele kwa alama kumi, moja mbele ya Mombasa Olympic FC.