Michezo

Kakamega High kujenga uwanja wa Sh120 milioni

June 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHULE ya Upili ya Kakamega imeanza mchakato wa kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kubeba mashabiki 10,000 walioketi katika juhudi za kujiandaa kwa fainali za Michezo ya Shule za Afrika Mashariki baadaye mwaka huu.

Mradi huo ambao umefadhiliwa na wanafunzi wa zamani wa Kakamega High, jamii na wahisani; umekadiriwa kugharimu kima cha Sh120 milioni. Ujenzi utashughulikuwa kwa awamu tatu. Awamu ya pili itaanza kutekelezwa chini ya kipindi cha majuma machache yajayo.

Ua utakaozingira uwanja huo ambao utakuwa na uwezo wa kuandaa michezo ya soka, hoki, voliboli, riadha, uogeleaji, mpira wa vikapu na netiboli; utakuwa wa kuta za saruji. Utakuwa pia na mahali pa mashabiki, wachezaji wa akiba na maafisa wa benchi za kiufundi kukalia pamoja na vyumba vya wachezaji kubadilishia sare.

Vyumba vya mazoezi ya viungo, kumbi za burudani, sehemu za watoto kuchezea, vyoo vipya na maegesho ni kati ya maeneo yatakayokuwa na sura mpya katika uga huo utakaowekewa zulia jipya la kisasa.

Kwa mujibu wa Isaac Kwoba ambaye ni mwenyekiti wa Green Commandos, uwanja huo utafaidi eneo zima la Magharibi ya Kenya na kuwa kitega-uchumi kwa kikosi chao.

“Awamu ya kwanza ya mradi huo ilikuwa ni ujenzi wa ua kabla ya kuwekwa kwa taa kisha vyumba vya wachezaji kubadilishia sare. Shughuli za kuweka viti kwenye eneo la mashabiki kukalia tayari inaendelea. Huo utakuwa mwisho wa awamu ya kwanza,” akatanguliza.

“Mwishoni mwa mradi, tunapania kuwa na uwanja wa mpira wa vikapu, bwawa la kisasa la viwango vya kimataifa na eneo la wanariadha kukimbilia,” akasema Kwoba huku akitaka serikali ya kaunti ya Kakamega na wahisani wengine zaidi kujitokeza kuwapiga jeki.

Kwa mtazamo wake, ustawi wa kikosi cha Green Commandos utategemea jinsi uwanja wao mpya utakavyosimamiwa.

“Tumewekeza pakubwa katika makuzi ya talanta miongoni mwa wanasoka chipukizi. Sasa tumeona haja ya kuweka miundo-misingi itakayoletea mapato kwa kikosi chetu ambacho tunazamia kianze kushiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hivi karibuni,” akaongeza.

Green Commandos kwa sasa wanashiriki Ligi ya Divisheni ya Kwanza ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).