Michezo

Kalimoni United FC yapiga hatua licha ya visiki

March 18th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

TIMU ya Kalimoni United FC ni timu yenye malengo makubwa ya kuinua maisha ya wanasoka wake katika eneo la Juja Kaunti ya Kiambu.

Kocha wake Martin Mwangi, anasema licha ya kupitia changa moto kadha, timu hiyo ina wachezaji wapatao 24 ambao wamejitolea mhanga kufanikisha malengo yao.

“Vijana wangu ni wenye nidhamu ambapo mazoezi yao ikatika Uwanja wa Premier Bag, Juja kati ya Juamtatu na Ijumaa majira ya saa 11 na 12 unusu za jioni,” anasema Kocha Mwangi.

Anasema Jambo linalowapiga chenga ni ukosefu wa vifaa muhimu vya kuchezea wanapotua Uwanjani. Anavitaja vifaa hivyo kama Jezi, viatu na mipira.

“Ama kwa kweli tumejaribu kutafuta usaidizi wa kutuweka mbele kwa kuwa na vifaa bora lakini bado wahisani wanatuonyesha kisogo bila kujitokeza wazi. Iwapo tungekuwa na vifaa muhimu bila shaka kikosi changu kingekuwa mbali,” alisema Mwangi.

Anasema timu hiyo imekuwa na uhai wake kwa miaka mitatu hivi lakini mara nyingi wao hutegemea mechi za mataji na za kirafiki.

“Tungetamani kupiga hatua na kucheza mechi za Ligi ya Kaunti Ndogo ya Thika, lakini uwezo wa hela ndicho kikwazo kikubwa kwetu. Tumejaribu kubisha afisi kadha kutafuta usaidizi lakini cha muhimu tunachopata ni ahadi zisizo na matunda,” alisema Mwangi, na kuongeza lakini vijana wangu wamesema hawatakufa moyo kwani bahati itakapogonga watafanikiwa.

Anasema wakati wa mwanzo alipoanza kunoa vijana hao alipata changa moto tele kwa sababu wengi wao walikosa kufika mazoezi kila mara huku wakionekana kuvunjika moyo jinsi mambo yalivyowaendea. Lakini baada ya kuwapa motisha walielewa umuhimu wa kuhudhuria mazoezi.

Katika mechi za kirafiki walizocheza hivi karibuni Kalimoni United iliikomoa Juja Farm FC kwa mabao 2-0. Vijana hao walitoka sare na Gachororo Stars kwa kulimana mabao 2-2. Hapo awali Timu hiyo iliikomoa Ndarugu Stars kwa mabao 2-1. Halafu waliweza kuilaza Murera Youth kwa mabao 2-0.

Mwangi anaomba taasisi zote na washika dau katika sekta ya soka Kaunti ya Kiambu kujitokeza na kudhamini vijana wake ili kumpunguzia mzigo wa kuendeleza talanta ya vijana hao .Baadhi ya timu wanazotarajia kupambana nazo kwa zoezi la kujiongeza ujuzi ni JKUAT FC, Githunguri Stars, Ruiru United FC na Angaza FC

“Tukicheza na timu hizo bila shaka tutakuwa na taswira nzuri jinsi tunavyoendeleza kikosi chetu,” alisema Mwangi.

Anasema jambo linalomtia hofu kila mara ni kwamba wakati mwingi wachezaji wake hupata majeraha na huchukua muda kabla ya mchezaji kupona vyema . Maswala ya matibabu pia ni changa moto lingine kwake.