Kampeni za Diamond League msimu ujao kuanzia Rabat, Morocco
Na CHRIS ADUNGO
WARATIBU wa mbio za Diamond League wamefichua kalenda ya mashindano hayo katika msimu ujao wa 2021.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kampeni hizo zitajumuisha duru 14 za riadha zitakazoanzia jijini Rabat, Morocco mnamo Mei na kumalizikia Zurich, Uswisi mnamo Septemba.
Jiji la Doha nchini Qatar litakuwa mwenyeji wa duru ya Mei 28 kabla ya Roma nchini Italia kuandaa duru ya Juni 4, kisha Oslo nchini Norway (Juni 11). Duru za Stockholm, Monaco na London zimeratibiwa kufanyika katika kipindi cha majuma mawili ya mwanzo wa Julai.
Baada ya likizo ya mwezi mmoja itakayopisha Olimpiki za Tokyo nchini Japan, mashindano ya Diamond League yatarejelewa kwa duru ya Shanghai mnamo Agosti 14 kabla ya Eugene (Agosti 21) kisha China iandae duru nyingine kwa mara ya pili mnamo Agosti 22.
Duru za mwisho zitafanyika barani Ulaya katika majiji ya Lausanne, Paris na Brussels kabla ya fainali ya msimu kufanyika Zurich kati ya Septemba 8-9.
Kwa mujibu wa waandalizi wa mbio za Diamond League, ratiba iliyotolewa kwa minajili ya kampeni za msimu wa 2021 si ya mwisho na huenda ikabadilika kutegemea hali ya maambukizi ya virusi vya corona duniani.
Kutoandaliwa kwa mbio zozote za nyika hadi kufikia sasa kulichangia matokeo mseto yaliyosajiliwa na Wakenya kwenye duru mbili za ufunguzi wa kivumbi cha Diamond League mnamo 2020.
Haya ni kwa mujibu wa kocha wa timu ya taifa ya riadha, Julius Kirwa ambaye ameshikilia kwamba mbio za nyika zimekuwa zikiwapa wanariadha wa humu nchini jukwaa mwafaka la kujiandalia kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa kila msimu.
“Kihistoria, mbio za nyika zimekuwa zikiwapa Wakenya stamina na uthabiti wa kutamba katika mashindano yote mengine yanayofuatia kila msimu. Kutokuwepo kwa mbio hizo muhula huu kulichangia mseto wa matokeo yaliyoandikishwa na Wakenya jijini Monaco nchini Ufaransa na Stockholm, Uswidi,” akatanguliza.
Kilele cha msimu wa mbio za nyika mwaka huu kingekuwa kuandaliwa kwa kivumbi cha Afrika nchini Togo mnamo Aprili. Hata hivyo, janga la corona lilichangia kuahirishwa kwa mbio hizo mnamo Machi.
Bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri alitawala fani hiyo kwenye kivumbi cha Diamond League jijini Monaco (14:22.12) kabla ya kuambulia nafasi ya 11 jijini Stockholm katika mbio za mita 1,500 kwa muda wa dakika 4:10.53.
Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chepkoech aliibuka wa sita jijini Stockholm katika mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 14:55.01 huku Ferguson Rotich akimaliza wa nne (1:45.11) katika mbio za mita 800.
Timothy Cheruiyot ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za 1,500 ndiye wa pekee aliyedumisha umahiri wake kwa kuibuka mshindi wa fani hiyo katika duru zote mbili za Diamond League.
Ingawa hivyo, Kirwa anaamini kwamba matokeo ya Wakenya yangeimarika zaidi katika duru za Brussels, Ubelgiji (Septemba 4), Naples, Italia (Septemba 17), Doha, Qatar (Septemba 25) na China (Oktoba 17).
“Ni matumaini yetu kwamba corona itadhibitiwa vilivyo hivi karibuni ndipo tuanze msimu wa mbio za nyika kabla ya msimu ujao wa Diamond League. Hilo litawapa wanariadha, hasa katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 jukwaa mwaridhawa zaidi la kujifua pia kwa Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan,” akasema.
RATIBA YA DIAMOND LEAGUE 2021:
Rabat – Mei 23
Doha – Mei 28
Roma – Juni 4
Oslo – Juni 10
Stockholm – Julai 4
Monaco – Julai 9
London – Julai 13
Shanghai – Agosti 14
Eugene – Agosti 21
China – Agosti 22
Lausanne – Agosti 26
Paris – Agosti 28
Brussels – Septemba 3
Zurich – Septemba 8-9