Michezo

Kamworor apigiwa upatu kuwa mwanariadha bora wa muda wote duniani katika Nusu Marathon

October 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

GEOFRREY Kamworor anapigiwa upatu na Shirikisho la Riadha Duniani (WA) kumdengua Zersenay Tadese wa Eritrea na kutawazwa mwanariadha bora wa muda wote duniani katika mbio za Nusu Marathon.

Bingwa huyu mara tatu wa katika Nusu Marathon ya Dunia, ni miongoni mwa Wakenya watatu ambao wamejumuishwa kwenye orodha ya nguli watano wanaowania taji hilo katika mbio za kilomita 21.

Wakenya wengine katika orodha hiyo ni Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOCK), Paul Tergat na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon kwa upande wa wanawake, Tegla Loroupe.

Tadese na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika marathon za wanawake, Paula Radcliffe wa Uingereza ndio wanariadha wengine wanaoikamilisha orodha hiyo.

“Iwapo Tadese ndiye mwanariadha bora zaidi wa muda wote kwenye nusu marathon, basi Kamworor huenda akamdengua na kuvikwa taji hilo. Kamworor ameibuka mfalme mara tatu wa mbio hizo za kilimoita 21 chini ya kipindi kifupi kilichopita,” ikasema sehemu ya taarifa ya WA.

Tadese almaarufu ‘Mr Half Marathoner’, anajivunia ubingwa wa mataji matano mfululizo katika mbio za nusu marathon, rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa na mwanariadha yeyote katika miaka ya hivi karibuni.

“Tadese ana uwezo mkubwa wa kuwapiku washindani wake kisaikolojia. Vipimo vya afya alivyofanyiwa vilibaini kwamba kinyume na washindani wake wakuu, yeye huhitaji kiwango kidogo zaidi cha oksijeni kwa kila kilomita akiwa mbioni,” ikaendelea sehemu ya taarifa.

Tadese anajivunia ufanisi wa kuweka rekodi mbili za dunia katika mbio za kilomita 21, ikiwemo ile ya dakika 58:23 aliyoiweka jijini Lisbon, Ureno mnamo 2010. Rekodi hiyo haikuvunjwa na mwanariadha yeyote kwa miaka minane.

Iwapo Kamworor atapania kuwa mrithi wa Tadese na kuweka hai ubashiri wa WA, basi atahitajika kujinyakulia mataji mawili zaidi ya mbio za Nusu Marathon Duniani.

Ukubwa wa uwezo wa Kamworor kwenye nusu marathon ulianza kudhihirika mnamo 2014 nchini Denmark alipokamilisha mbio Copenhagen kwa muda wa saa 1:00:02.

Aliboresha muda huo zaidi miaka miwili baadaye jijini Cardiff kwa kukata utepe baada ya dakika 59:10. Ushindi wake jijini Cardiff, Uingereza ulimvunia sifa na umaarufu hasa ikizingatiwa kwamba alianza mbio hizo vibaya baada ya kuteleza na kupoteza jumla ya sekunde 15.

Aliibuka mshindi wa Nusu Marathon za Dunia kwa mara ya mwisho mnamo 2018 kabla ya kutawala mbio za New York Marathon Marathon mnamo 2019 kwa muda wa saa 2:08:13.

Kamworor hakuwa sehemu ya kikosi kilichopeperusha bendera ya Kenya kwenye makala ya 24 ya Riadha za Nusu Marathon Duniani mjini Gdynia, Poland mnamo Oktoba 17, 2020.

Kutokuwepo kwake kulisaza Kenya katika ulazima wa kutegemea Morris Munene Gachaga, Bernard Kipkorir Ng’eno, Bernard Kimeli, Leonard Barsoton na Kibiwott Kandie aliyeambulia nafasi ya pili (58:54) nyuma ya Jacob Kiplimo wa Uganda (58:49). Ushindi huo wa Kandie ulimvunia kima cha Sh1.6 milioni.

Kamworor atalenga sasa kujinyanyua na kutawala mbio za nyika duniani zitakazoandaliwa mjini Bathurst, Australia mnamo 2021.