Kamworor azoa Sh2.8 milioni baada ya kuvunja rekodi
Na GEOFFREY ANENE
BINGWA mara tatu wa Riadha za Nusu-Marathon Duniani, Geoffrey Kamworor ni mshikilizi wa rekodi mpya ya dunia ya mbio za kilomita 21 baada ya kutwaa taji la Copenhagen Half Marathon kwa dakika 58:01 nchini Denmark, Jumapili.
Alitia mfukoni Sh1.0 milioni kwa ushindi, Sh1.0 milioni kwa rekodi ya dunia, Sh518,550 kwa rekodi mpya ya Copenhagen Half Marathon na Sh207,420 kwa kukamilisha umbali huo chini ya dakika 60 kabla ya ushuru wa asilimia 15 kutolewa.
Kwa jumla alizoa takribani Sh2.8 milioni kabla ya ushuru huo
Kamworor, aliyetumia mbio za Copenhagen kujiandaa kurejesha taji la mbio za kilomita 42 za New York, zitakazofanyika nchini Marekani hapo Novemba 3, alilopoteza mwaka jana, alifuta rekodi ya Mkenya mwenzake Abraham Kiptum ya dakika 58:18 iliyowekwa mjini Valencia nchini Uhispania mnamo Oktoba 28, 2018.
Mkimbiaji huyu aliyebeba mataji ya dunia ya Half Marathon mwaka 2014, 2016 na 2018, alichupa uongozini mjini Copenhagen baada ya kilomita 11 na kujiweka pazuri kuvunja rekodi alipopita kilomita 13 kwa dakika 35:40, kilomita 15 kwa dakika 41:05 na kilomita 20 kwa dakika 55:00.
Kamworor aliingia mbio za Copenhagen muda wake bora katika nusu marathon ukiwa dakika 58:54 aliotimka akitwaa taji la Ras Al Khaimah mwaka 2013.
Mbali na kuvunja rekodi ya dunia, muda wa Kamworor pia ulifuta rekodi ya Copenhagen Half Marathon ya dakika 58:40 iliyowekwa na Mbahraini Abraham Cheroben, ambaye ni mzawa wa Kenya, mwaka 2017.
Kamworor alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Benard Kipkorir Ng’eno (dakika 59:16), Muethiopia Berehanu Tsegu (59:22) na Wakenya Edwin Kiptoo (59:27), Amos Kurgat (59:37), Philemon Kiplimo (59:57) na Shadrack Koech (saa 1:00:12), mtawalia.
Kabla ya Kamworor, Wakenya Bedan Karoki, James Wangari na Daniel Kipchumba walikuwa wametwaa mataji ya Copenhagen mwaka 2015, 2016 na 2018, mtawalia.
Wanawake
Taji la wanawake lilinyakuliwa na raia wa Ethiopia, Birhane Dibaba kwa saa 1:05:57 akifuatiwa unyounyo na Wakenya Evaline Chirchir (1:06:22), Dorcas Tuitoek (1:06:36), mtawalia. Purity Rionoripo anasalia Mkenya wa pekee kushinda taji la wanawake la Copenhagen Half Marathon. Aliibuka mshindi mwaka 2015.
Rekodi mpya ya mbio za kilomita 21 ya wanaume iliwekwa wiki moja baada ya Mkenya Brigid Kosgei kuweka rekodi mpya ya wanawake ya dakika 64:28 kwenye mbio za Great North Run nchini Uingereza, ambayo hata hivyo Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) lilithibitisha kuwa halitaitambua kwa sababu sehemu ya mashindano haikutimiza masharti yanayohitajika kufanya hivyo.