Kamworor kuongoza kikosi cha nusu marathon Poland
Na MWANDISHI WETU
BINGWA mtetezi Geoffrey Kamworor na mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za kilomita 21 duniani, Pauline Kaveke wataongoza kikosi cha Kenya katika makala ya 24 ya Nusu Marathon ya Dunia mnamo Machi 29 mjini Gdynia, Poland.
Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limemteua Kamworor ambaye atakuwa akiwania ubingwa wa mbio hizo kwa mara ya nne mfululizo kuwa kinara wa timu ya wanaume inayomjumuisha pia Kibiwott Kandie. Kandie alitiwa kikosini mwezi mmoja baada ya kuibuka mshindi wa Nusu Marathon ya Ras Al Khaimah (RAK) iliyoandaliwa mwezi jana katika Nchi za Milki za Kiarabu (UAE).
Kabla ya kutua UAE alikotawala Ras Al Khaimah Half Marathon mnamo Februari 21, Kandie alikuwa amemshinda Kamworor mnamo Februari 15 mjini Ngong na kunyanyulia kikosi chake cha KDF medali ya kwanza ya Mbio za Nyika za Kitaifa baada ya miaka 17.
Kamworor ambaye ni bingwa wa dunia katika Nusu Marathon, alitawazwa mshindi wa mbio hizo kwa mara ya tatu mnamo 2018 jijini Valencia, Uhispania. Hii ni baada ya kuzidi maarifa mwanariadha mzawa wa Kenya na raia wa Bahrain, Naibei Cheroben na Aron Kifle wa Eritrea walioambulia nafasi za pili na tatu mtawalia.
Kamworor aliweka muda bora zaidi wa binfasi wa dakika 58:01 mnamo Septemba 15, 2019 baada ya kuibuka mshindi wa Nusu Marathon ya Dunia jijini Copenhagen, Denmark.
Kwa upande wake, mbio za RAK zilimpa Kandie jukwaa mwafaka zaidi wa kuweka muda bora wa binafsi wa dakika 58:58 mnamo Februari 21, 2020.
Mtimkaji mwingine aliyetiwa katika kikosi cha wanaume kilichofichuliwa na Naibu Rais wa AK Paul Mutwii ni mshindi wa medali ya fedha katika Mbio za Nyika Dunia mnamo 2017, Leonard Barsoton. Barsoton aliyekamata nafasi ya 12 jijini Valencia mnamo 2018, aliambulia nafasi ya sita katika Nusu Marathon ya RAK mwezi jana.
Shadrack Kimining aliyeambulia nafasi ya tatu katika Houston Half Marathon mnamo Januari 2020 na Victor Chumo aliyeshikilia nafasi ya tatu katika Guadalajara Half Marathon mnamo Februari pia wamo katika kikosi cha Kenya kwa upande wa wanaume.
Kimining aliyeibuka mshindi wa Peterborough Half Marathon mnamo 2016 anajivunia muda bora wa dakika 59:27 aliouweka katika Houston Half Marathon mwanzoni mwa mwaka huu. Mwanariadha huyo aliwahi pia kutawala mbio za Cardiff Half Marathon nchini Uingereza mnamo 2016.
Chumo aliyekuwa miongoni mwa wanariadha waliodhibiti kasi ya Eliud Kipchoge wakati wa mbio za Ineos 1:59 Challenge mwaka jana, anajivunia muda bora wa dakika 59:58 aliouweka alipoibuka mshindi wa Barcelona Half Marathon mnamo Februari 16, 2020.