Michezo

Kandarasi ya Migne yakatizwa

August 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MASHINDANO makubwa huwa katili kwa makocha wa timu za taifa na mambo hayajakuwa tofauti baada ya matokeo ya Kombe la Afrika (AFCON) kuchangia pakubwa katika kutimuliwa kwa makocha 10 waliokuwa nchini Misri kwa makala hayo ya 32.

Kocha Sebastien Migne, ambaye aliongoza Kenya kurejea katika Afcon kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004, ameungana na raia wa Mexico Javier Aguirre (Misri), Mnigeria Emmanuel Amunike (Tanzania), Ricardo Mannetti (Namibia), Mholanzi Clarence Seedorf (Cameroon), Mbelgiji Paul Put (Ubelgiji), Mfaransa Sebastien Desabre (Uganda), Mfaransa Herve Renard (Morocco), Sunday Chidzambga (Zimbabwe) na Muingereza Stuart Baxter (Afrika Kusini) walioachishwa kazi ama kujiuzulu wenyewe mapema mapema.

Ripoti nchini Angola pia zinasema kuwa ni muda tu kabla ya raia wa Serbia Srdjan Vasiljevic akuangukiwa na shoka.

Migne, ambaye kandarasi yake na Kenya ilianza Mei 1 mwaka 2018 na kutarajiwa kutamatika Juni 30 mwaka 2021, sasa ni aliyekuwa kocha mkuu wa Harambee Stars baada ya kuafikiana na Shirikisho la Soka nchini (FKF) kukatiza kandarasi hiyo.

Mfaransa huyu, ambaye amekuwa akikosolewa na Wakenya sana kutokana na uteuzi wake wa timu ya Afcon 2019, amekuwa akilipwa mshahara wa Sh1.5 milioni kila mwezi. Atalipwa fidia kwa awamu, FKF ilisema Agosti 12.

Wiki chache zilizopita Wakenya walibashiri kuwa ni muda tu kabla ya Migne kupigwa teke baada ya Francis Kimanzi kuagana na Mathare United. Walisema Kimanzi kuachana na Mathare kabisa ni ishara kuwa FKF ilikuwa ikimuandaa kocha huyo wa zamani wa Kenya kujaza nafasi ya Mfaransa huyo.

Migne aliongoza Kenya katika mechi 15 zikiwemo tatu katika fainali za Afcon 2019 nchini Misri alikoandikisha vichapo viwili dhidi ya Algeria (2-0) na Senegal (3-0) na ushindi dhidi ya Tanzania (3-2) katika mechi za makundi.

Stars ilikuwa inarejea katika Afcon baada ya kuwa nje miaka 15. Mara ya mwisho Migne aliongoza Stars ilikuwa wiki chache zilizopita katika mechi ya kufuzu kushiriki soka ya Afrika ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao (CHAN). Stars ilikabwa 0-0 Julai 28 jijini Dar es Salaam na kuandikisha matokeo sawia katika mechi ya marudiano mnamo Agosti 4 na kubanduliwa nje ya majirani hao kwa njia ya penalti 4-1 uwanjani Kasarani.

“FKF inafanya mipango ya kuteua benchi mpya la kiufundi kuongoza Harambee Stars. Kocha mpya atajulikana hivi karibuni. Tunamtakia kila la kheri tunapoagana naye na kuelekeza malengo yetu katika mechi za kufuzu kushiriki Afcon mwaka 2021 zinazokaribia kuanza,” taarifa kutoka FKF ilisema.