• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kangemi Ladies wahifadhi taji la NWRL

Kangemi Ladies wahifadhi taji la NWRL

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kangemi Ladies imehifadhi taji la Nairobi West Regional League (NWRL) huku ikiwa imesalia mechi moja kukamilisha ratiba ya ngarambe hiyo msimu huu. Kangemi Ladies ya kocha, Loice Karanja amkaa mkao wa subira kutawazwa mabingwa wa kipute hicho baada ya kuweka pengo la pointi nane baina yake na Uweza Women.

Wasichana wa Kangemi Ladies walithibitishwa kubeba taji hilo waliponasa alama nne licha ya kwamba walipania kuzoa pointi sita baada ya kucheza mechi mbili. Vigoli hao waliichoma Uweza Women magoli 3-0 kisha kutoka nguvu sawa mabao 2-2 na Carolina For Kibera(CFK) katika uwanja wa shule ya msingi ya Toi Kibera, Nairobi.

Kwenye mechi hizo, Kangemi Ladies ilishusha mchezo safi na kuhakikisha imeliza Uweza Women kwa mara ya pili kwenye kipute cha msimu huu. Sorophine Ajiambo na Drailer Salome kila mmoja alifungia Kangemi Ladies mabao mawili huku Fasila Adhiambo akitikisa wavu mara moja.

Magoli ya CFK yalipatikana kupitia Mercy Mwachi na Melvin Kirisha waliopiga moja kila mmoja. ”Katika mpango mzima napongeza wachezaji wangu ambao tangia tulipoanza mechi za msimu huu wameonyesha wamepania makubwa dimbani,” kocha wa Kangemi Ladies alisema na kuongeza kuwa hata Uweza Women ikishinda mchezo wa mwisho kamwe haiwezi kuwafikia.

Matokeo mengine, Uweza Women ilipata ushindi wa kijifariji ilipovuna mabao 2-0 dhidi ya City Queens kupitia Janet Kazungu na Marion Andesia waliopiga moja safi kila mmoja. Nayo Amani Queens ilijikuta njiapanda walipokubali kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Lifting The Bar.

Kangemi Ladies inaongoza kwa kukusanya alama 30, sita mbele ya Uweza Women baada ya kucheza mechi 12 kila mmoja. Mechi za kukunja jamvi zimepangwa kupigwa wikendi hii kwenye viwanja tofauti katika Kaunti ya Nairobi. Kipute cha msimu huu kinajumuisha:Uweza Women, Kangemi Ladies, Kibagare Girls, Carolina For Kibera(CFK), Lifting The Bar, Amani Queens, The UoN Queens na City Queens.

You can share this post!

Mbotela Kamaliza yakosa taji

Kuria akataa marupurupu, aamuru pesa hizo zipelekwe...

adminleo