Kapenguria Heroes wajiandalia Chapa Dimba
Na JOHN KIMWERE
WALIOKUWA mabingwa wa Chapa Dimba na Safaricon Season One, kitengo cha wavulana Kapenguria Heroes katika Mkoa wa Rift Vallley ni miongoni mwa vikosi nane vitakavyoshiriki fainali za kipute hicho Season Three wikendi hii.
Fainali za mwaka huu zitachezewa katika uwanjani Green Stadium, mjini Kericho.
Vile vile wavulana wa Al-Ahly kutoka Kajiado waliomaliza nafasi ya pili katika fainali za kitaifa mwaka jana watakosekana katika fainali za mwaka huu.
Kwa kina dada waliokuwa mabingwa kitengo hicho, Kitale Queens walipata ushindani mkali na kushindwa kufuzu kushiriki fainali za mwaka huu.
Kwenye mechi za nusu fainali za wavulana Kapenguria ya Pokot Magharibi italimana na White Rhino kutoka Transmara.
Kapenguria Heroes itakuwa mbioni kutetea taji hilo ililopokonywa mwaka uliyopita. Nao wenzao Laiser Hill Academy kutoka Kajiado imepangwa kukwaruzana na Tumkas FC kutoka Uasin Gishu.
Katika kitengo cha wasichana, Itigo Girls kutoka Nandi Kaskazini itapepetana na Achievers kutoka Kajiado huku Bomet Queens ikimenyana na Wiyeeta kutoka Pokot Magharibi.
”Mechi za muhula huu zinaonyesha ushindani wa kufa mtu ambapo imekuwa vigumu kutofautisha kama ni michezo ya viwango vya chini wengi wanadhania ni fainali za kitaifa,” alisema mshirikishi wa kipute hicho wa Safaricom, Evans Omondi.
”Soka halina heshima kabisa. Wachezaji wanaweza kufika uwanjani wakiwa tayari kufanya kweli na kushinda mechi lakini washindwe kutimiza azimio hilo.
“Hatuwezi kusema lazima tuibuke washindi lakini tunatarajia kujikaza tuwezavyo kwenye juhudi za kupigania taji la msimu huu,” alisema kocha wa Tumkas FC, Peter Tanui.
Mwaka jana, Kitale Queens ilishinda Itigo Girls kwa mabao 4-0 na kutwaa ubingwa huo kisha ilikomoa Acokoro Ladies mabao 4-2 kupitia penalti katika fainali za kitaifa na kutawazwa malkia.
Katika fainali za eneo hilo kwa wavulana Al-Ahly ilitawazwa mabingwa baada ya kulima Tumkas FC mabao 3-0 lakini ililemewa na Manyatta United katika fainali za kitaifa.
Mabingwa wa taji hilo, kitengo cha wavulana na wasichana watajikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ambazo zimepangwa kuandaliwa mjini Mombasa Mwezi Juni mwaka huu.
Kando na hayo, timu hizo mbili kila moja itapokea kitaita cha Sh200,000. Nazo timu zitakaomaliza katika nafasi mbili kila moja itapoongezwa kwa Sh100,000.
Washindi wa eneo hilo watajiunga na wenzao kutoka maeneo mengine kufuzu kwa fainali za kitaifa. Wavulana watajiunga na wenzao wa Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati , Dagoretti Mixed (Mkoa wa Nairobi),
Tumaini School (Mkoa wa Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa. Wasichana watajiunga na Falling Waters Mkoa wa Kati, Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.