KARANTINI: Kocha kukosa mechi ya Bundesliga kwa kununua dawa ya meno
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Mkuu wa Augsburg, Heiko Herrlich atakosa mechi ya kwanza ikakayoshuhudia Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ikirejelewa mnamo Mei 16, 2020.
Hii ni baada ya mkufunzi huyo kuvunja kanuni za karantini kwa kuondoka katika hoteli ya kikosi chake kwenda kununua dawa ya meno.
Akizungumza na wanahabri, Herrlich ambaye kikosi chake kinatazamiwa kukutana na Wolfsburg mnamo Mei 16, 2020 alisema kwamba alijikuta hana dawa na meno na akalazimika kuvunja kanuni zinazowadhibiti hotelini kwenda katika mojawapo ya maduka ya jumla karibu na wanakoishi.
Vikosi vya Bundesliga vimekuwa vikishiriki mazoezi na wachezaji kutengwa mara kwa mara kadri wanavyojiandaa kwa marejeo ya soka ya Ujerumani.
“Nilikosea kwa kutoka hotelini,” akasema Herrlich katika taarifa yake.
Herrlich, 48, alipokezwa mikoba ya Augsburg mnamo Machi 10 na mechi dhidi ya VfL Wolfsburg ilikuwa iwe yake ya kwanza kusimamia mnamo Mei 16, 2020.
“Ingawa nimefuata masharti yote mengine ya kudumisha afya nikiwa ndani au nje ya hoteli,hili ni tukio ambalo siwezi kabisa kulieleza nikaeleweke. Katika hali iliyonipata, sidhani nilifanya vyema na siwezi kabisa kuwa kilelezo chema kwa kikosi change au umma,” akatanguliza.
“Hivyo, itanilazimu kujirekebisha na kuuungama kosa langu. Kwa sababu ya nimekosea, sitaweza kuongoza kikosi cha vipindi vijavyo vya mazoezi hadi kitakaposhuka dimbani kuvaana na Wolfsburg mnamo Jumamosi ya Mei 16,” akasema Herrlich.
Vinara wa Augsburg wamesema kwamba wachezaji na maafisa wote wa kikosi huwa wanafanyiwa vipimo vya mara kwa mara kubaini iwapo wana virusi vya corona au la. Herrlich ataruhusiwa tu kuungana na wanasoka wake katika kambi ya mazoezi baada ya kupimwa mara mbili na kutopatikana na virusi vya corona.
Hadi kipute cha Bundesliga kilipositishwa kwa muda mnamo Machi 2020, Augsburg walikuwa wakishikilia nafasi ya 14 jedwalini kwa alama 27, tano pekee nje ya mduara hatari wa kuteremshwa ngazi.