Michezo

Kashiwa Reysol anayochezea Olunga yagawana alama na Hiroshima

September 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KASHIWA Reysol imeambulia alama moja katika sare ya 1-1 dhidi ya Sanfrecce Hiroshima kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Japan ambayo mshambuliaji Michael Olunga alipoteza nafasi ya wazi Jumamosi.

Mvamizi Mbrazil Douglas Vieira aliweka wageni Hiroshima kifua mbele dakika ya tisa baada ya kupokea mpira kutoka kiungo Yoshifumi Kashiwa.

Reysol ilisawazisha 1-1 kupitia kwa Kengo Kitazume sekunde chache kabla ya kipindi cha kwanza kukatika baada ya beki huyo kupokea pasi murwa kutoka kwa kiungo Ataru Esaka.

Olunga, 26, ambaye alikuwa amefunga mabao katika mechi tatu mfululizo, alipoteza nafasi nzuri dakika chache kabla ya bao la Kitazume alipochenga kipa, lakini shuti lake likaondoshwa na beki.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya anasalia juu ya orodha ya wafungaji kwenye ligi hiyo ya klabu 18 kwa mabao 16. Alikuwa amefungua mwanya wa magoli sita alipotikisa nyavu mara moja Kashiwa ikilemewa 2-1 na Sagan Tosu katika mechi iliyopita.

Baada ya michuano ya Septemba 19, mwanya huo sasa umepunguzwa na goli moja. Hii ni baada ya Mbrazil Everaldo kufungia Kashima Antlers bao moja ikicharaza Cerezo Osaka 2-1. Mbrazil Marcos Junior anashikilia nafasi ya tatu kwa mabao 10 baada ya kuongeza goli moja mabingwa watetezi Yokohama Marinos wakizaba Tosu 3-1.

Katika matokeo ya mechi zingine zilizosakatwa Jumamosi, Sapporo ilikubali kichapo cha 1-0 dhidi ya Gamba Osaka, Nagoya Grampus ikalaza Vissel Kobe anayochezea Mhispania Andreas Iniesta nayo Shonan ikanyolewa bila maji 3-0 dhidi ya Shimizu.

Viongozi Kawasaki Frontale watateremka uwanjani hapo Jumapili kuzichapa dhidi ya Urawa Red Diamonds. Kawasaki itafungua mwanya wa alama nane ikipiga Urawa baada ya nambari mbili Cerezo kuteleza dhidi ya Kashima. Reysol inashikilia nafasi ya sita kwa alama 27 kutokana na mechi 17.