Kashiwa Reysol yapepeta Ehime 2-1
Na GEOFFREY ANENE
KLABU ya Kashiwa Reysol, ambayo imeajiri Mkenya Michael Olunga, imemaliza mikosi ya mechi tatu bila ushindi kwa kupepeta Ehime 2-1 kwenye Ligi ya Soka ya Daraja ya Pili ya Japan uwanjani Hitachi Kashiwa, Jumapili.
Kashiwa iliingia mchuano huu ikiuguza kichapo cha mabao 4-3 dhidi ya Montedio Yamagata na kutoka sare za 1-1 dhidi ya Albirex Niigata na Kofu. Ilifaulu kulipiza kisasi cha kulimwa 3-1 na Ehime mwezi Juni kwa kufunga mabao hayo mawili muhimu kupitia kwa beki Yuta Someya dakika ya 60 na kiungo Ataru Esaka dakika ya 80.
Mshambuliaji Yoshiki Fujimoto aliweka Ehime kifua mbele dakika ya pili ya majehuri kabla ya kuenda mapumzikoni nayo Kashiwa ikajibu na mabao mawili katika kipindi cha pili kwenye mechi hiyo ya raundi ya 33 katika ligi hii ya klabu 22.
Kashiwa inaongoza kampeni za kuingia Ligi Kuu baada ya kuzoa alama 66. Viongozi hawa wako alama tisa mbele ya nambari mbili Yokohoma na nambari tatu Mito, ambao pia wamecheza mechi 33, na nambari nne Montedio Yamagata, ambayo itasakata mechi yake ya 33 hapo Jumatatu dhidi ya nambari 18 Ryukyu.
Olunga, ambaye hajaona lango katika mechi tano sasa, alichezeshwa na kocha Mbrazil Nelsinho Baptista mechi nzima.