Kaunti ya Nandi yamtuza Kipchoge ng'ombe, uwanja mpya kuitwa Eliud Kipchoge Sports Complex
Na GEOFFREY ANENE
BINGWA wa mara tatu wa mbio za kilomita 42 za Berlin nchini Ujerumani na London nchini Uingereza, Eliud Kipchoge amezawadiwa na Serikali ya Kaunti ya Nandi, ng’ombe jike kwa kuvunja rekodi ya dunia.
Mshindi huyu wa Olimpiki pamoja na malkia mara tatu wa Berlin Marathon Gladys Cherono, na bingwa wa Seoul Marathon mwaka 2017 Amos Kipruto waliandaliwa dhifa ya chakula cha asubuhi katika afisi za serikali ya kaunti ya Nandi ambako walipewa ng’ombe jike kila mmoja, huku Gavana Stephen Sang akitangaza pia serikali yake itaunda majengo mazuri na kuweka vifaa vya michezo na kuyapa jina Eliud Kipchoge Sports Complex na mengine kuitwa baada ya Gladys Cherono na Amos Kipruto. Eneo lenyewe litakuwa na uwezo wa kuwa na vitanda 200.
“Tunajenga sehemu mpya ya michezo itakayoitwa Eliud Kipchoge Sports Complex, ambayo itakuwa makao kwa wanariadha wanapofanya mazoezi,” amesema Sang’ akifichua kwamba kaunti hiyo haina mipango ya kubadilisha jina la uwanja wa Kipchoge Keino, ambao ulipata jina hilo kutoka kwa bingwa wa zamani wa Olimpiki wa mbio za mita 1,500 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji na Rais wa zamani wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya, Kipchoge Keino.
Eliud Kipchoge alishinda Berlin Marathon mwaka 2018 kwa saa 2:01:39, ambayo ni rekodi mpya ya marathon duniani. Alifuta rekodi iliyokuwepo ya saa 2:02:57, ambayo Mkenya mwenzake Dennis Kimetto aliweka akishinda Berlin Marathon mwaka 2014. Alirejea nyumbani kisiri Septemba 20 baada ya kutangazia yeyote atawasili siku hiyo kwa hivyo hakuandaliwa mapokezi ya kishujaa jinsi Shrikisho la Riadha la Kenya (AK) lilikuwa limepanga.
Kipruto alimaliza nyuma ya Eliud Kipchoge katika nafasi ya pili kwa saa 2:06:23 naye Wilson Kipsang’, ambaye ni bingwa wa zamani wa Berlin Marathon na pia mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia, akafunga tatu-bora kwa saa 2:06:48.