Kaunti ya Taita Taveta yakuza vipaji kwa kudhamini mashindano ya riadha
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta inayoongozwa na Gavana Andrew Mwadime imeweka historia mpya ya mchezo wa riadha katika Kanda ya Pwani kwa kutoa udhamini kamili wa Mbio za Nyika za kuanzia ngazi ya kaunti ndogo hadi ngazi ya kaunti.
Mbio za Nyika za mwaka 2024 zinazofahamika kwa jina la Wakujaa Cross Country zimedhaminiwa kikamilifu na gavana Mwadime kuanzia ngazi za kaunti ndogo za Voi, Mwatate, Taveta, na Wundanyi ambazo zilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wakujaa Cross Country ya ngazi ya Kaunti ya Taita Taveta inatarajiwa kufanyika hapo Jumamosi hii ambapo kuna matumaini makubwa kutachipuka mastaa wengine wapya ambao wataweza kufikia viwango vya wakimbiaji wawili kutoka kaunti hiyo walioshinda mbio za marathon za kimataifa.
Wanariadha hao ni Samwel Mailu kutoka kaunti ndogo ya Taveta aliyeibuka mshindi wa mbio za Vienna Marathon zilizofanyika April mwaka uliopita alipotumia muda wa saa 2:05:08 na Paul Mkungo kutoka kaunti ndogo ya Mwatate aliyeshinda Istanbul Marathon Novemba 2023 akitumia muda wa saa 2:10:35.
Kutokana na jinsi wanariadha hao wawili wanavyoendelea kuwika kwenye mbio kadhaa za kimataifa na baadhi ya chipukizi ambao wanavutia wadhamini, serikali ya Taita Taveta imeamua kusaidia Chama cha Riadha nchini (AK) cha tawi dogo la kaunti hiyo kwa kutoa udhamini wa mashindano hayo.
Waziri wa Michezo wa Kaunti ya Taita Taveta, Shadrack Mutungi, amesema serikali hiyo imeonelea ijitolee kudhamini mbio hizo za nyika kwa nia ya kuwasaidia wanariadha chipukizi kunoa vipaji vyao ili kaunti hiyo iwe na wakimbiaji wengi mahiri watakaotambulika kote duniani.
“Gavana Mwadime ana nia kubwa ya kuhakikisha kuwa mchezo wa riadha unawasaidia vijana kuinua viwango na vipaji vyao katika mchezo huo sawa na walivyo kina Mailu na Mkungo. Tuna nia ya kudhamini mbio hizi mwakani katika wadi zote kwani tunaamini kuna wakimbiaji wazuri mashinani,” akasema Mutungi.
Waziri huyo alisema udhamini wao hautakomea kwenye mbio za kaunti za Jumamosi kwani wataendelea kuidhamini timu ya wanariadha itakayochaguliwa kuwakilisha kaunti hiyo kwenye Mbio za Nyika za Kanda ya Pwani zitakazofanyika Malindi mnamo Februari 10.
“Tutakapomaliza mbio za Jumamosi, wale watakaochaguliwa kuwakilisha kaunti yetu kwenye mbio hizo za Kanda ya Pwani, tutagharimia kambi yao ya mazoezi ya siku nne kabla ya kuenda Malindi na huko tutaendelea kugharamia usafiri wao, malazi na chakula hadi watakaporudi nyumbani,” akasema Mutungi.
Alisema ni matumaini yao kuwa kutokana na udhamini watakaoutoa, utazalisha matunda na timu ya Taita Taveta itaendelea kutawala mchezo wa riadha katika Kanda ya Pwani.
“Tunataka wanariadha wetu washinde vitengo vyote vitakavyoshindaniwa huko Malindi,” akasema.
aye Mwenyekiti wa AK Taita Taveta, Dammy Kisalu, aliishukuru serikali ya kaunti hiyo kwa kuwapa udhamini kamili ambao ana uhakika utasaidia pakubwa kuwafanya wanariadha wanaoinukia kufanya vizuri kwenye mbio za kanda na hata za kitaifa.
Kisalu anasema mastaa wao–Mailu na Mkungo–hawatashiriki kwenye mbio hizo za kaunti kwa sababu watakuwa ng’ambo kushiriki mbio za kimataifa lakini watajumuika na wenzao watakaokuwa kambini kujiandaa kwa mbio za kanda.
“Tunamshukuru sana gavana Mwadime na maafisa wake kwa kukubali kutudhamini kikamilifu kwa mbio za kaunti ndogo na za kaunti pamoja na kugharamia safari ya kuenda Malindi kutetea mataji yetu ambayo nina imani kubwa tutarudi nayo nyumbani,” akasema Kisalu.