Michezo

Kaunti yageukia soka kunasua vijana kutokana na minyororo ya mihadarati

December 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA KALUME KAZUNGU

JUMLA ya timu 196 zitashiriki kwenye ligi maalum iliyozinduliwa ili kuhubiri amani, uwiano na utangamano miongoni mwa makabila Kaunti ya Lamu.

Ligi hiyo ambayo imegharimu serikali ya kaunti ya Lamu kima cha Sh 5 milioni pia inapania kuwanasua vijana kutoka kwa janga la mihadarati.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa ligi hiyo Alhamisi, Naibu Gavana wa Lamu, Abdulhakim Aboud, aliwataka wakazi hasa vijana kutumia fursa hiyo ili kuhubiri amani na pia kuepuka kujiingiza katika uraubu wa mihadarati.

Bw Aboud alisema kaunti itajitolea kwa kila hali ili kuona kwamba maisdha ya vijana yanainuliwa.

Alisema ili maendeleo kuafikiwa eneo hilo, ni lazima wakazi waungane kuhubiri amani, uwiano na utangamano.

“Madhumuni makuu ya kuzindua ligi hii ni kuwanasua vijana wetu kutoka kwa janga la mihadarati na kuwafanya mabalozi wa amani eneo hili. Tunataka amani, umoja, uwiano na utangamano wa makabila kuhubiriwa wakati wa mechi mbalimbali zitakazoandaliwa kupitia ligi hii tuliyozindua leo,” akasema Bw Aboud.

Naye Afisa Mkuu wa Idara ya Vijana, Jinsia, Michezo na Masuala yta Kijamii wa Kaunti ya Lamu, Bw Joseph Ng’ang’a, alisema ligi hiyo pia inalenga kutambua vipaji mbalimbali miongoni mwa vijana ili vipaji hivyo vikuzwe na kaunti na kuwanufaisha vijana katika maisha.

Bw Ng’ang’a alisema fainali ya ligi hiyo imepangwa kufanyika mnamo Disemba 23 mwaka huu.

Alisema ligi hiyo itashirikisha awamu za mwondoano kabla ya timu kumi kusalia kwenye ligi hiyo.

“Kwa sasa tumesajili timu 196 ambazo zimeanza kushiriki awamu ya mwondoano. Tunataka kubakia na timu kumi ambazo zitawakilisha wadi zote kumi za Lamu. Timu hizo zitakaa Mpeketoni kwa siku tatu ili kushiriki mechi za robo fainali na nusu fainali kabla ya fainali yenyewe kuandaliwa kufikia Disemba 23. Mshindi kwenye ligi hiyo atapata zawadi kemkem,” akasema Bw Ng’ang’a.