Michezo

Kayole Asubuhi waondolewa Super 8

October 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN ASHIHUNDU

KAYOLE Asubuhi FC imekuwa timu ya kwanza kuteremshwa ngazi kutoka kwa Ligi Kuu ya Super 8, na sasa mabingwa hao wa zamani watashiriki katika ligi ya chini msimu ujao.

Timu nyingine tatu zitashushwa hadi daraja la Kwanza baada ya mechi za kufunga msimu zitakazochezwa mwishoni mwa juma.

Kayole waliteremshwa mwishoni mwa wiki baada ya kutoka sare 1-1 na mabingwa wapya Jericho All Stars katika mechi ngumu iliyochezewa uwanja wa Calvary.

Huku ikibakisha mechi moja, Asubuhi ambao wamejikusanyia jumla ya pointi 27 wanaweza tu kufikisha pointi 30 nyuma ya Shauri Moyo Blue Stars walio na 32 na RYSA (31). Walishinda mechi sita, kwenda sare mara katika mechi 29.

Huku wakishangiliwa na mashabiki wengi wa nyumbani, Asubuhi walipoteza nafasi nyingi za kufunga baada ya kutangulia kuona lango kupitia kwa Godwin Sematimba aliyefunga dakika ya 28 kupitia kwa mkwaju wa penalti.

Jericho ambao walitawazwa mabingwa mapema walisawazisha dakika ya 66 kupitia kwa bao la Kelvin Ndung’u ambaye amefunga jumla ya mabao 24 goals.

“Umekuwa msimu mgumu kwetu; tunajaribu kuunda kikosi kipya baada ya kusajili wachezaji kadhaa wapya ambao hawajaanza kuelewana vyema,” kocha wa Isaiah Omondi alisema. “Tumeshuka kutokana na shida mbali mbali, lakini tutarejea hivi karibuni,” aliongeza.

Ugani Ziwani, Blue Stars walitegemea bao la Erick Kyalo katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya RYSA.

Huku wakijivunia nafasi ya 12, Blue Stars wako na pointi 32 sawa na Zamalek ambao walishindwa 0-4 na TUK na Metro Sports ambao walitoka sare 1-1 na Meltah Kabiria.

Kutokana na jinsi hali ilivyo, lazima Blue Stars na RYSA zipate ushindi katika mechi zao za mwisho, la si hivyo zitafuata Kayole.

Matokeo ya mechi za mwishoni mwa wiki yalikuwa:

Shauri Moyo Blue Stars 1-0 RYSA; Kawangware United 3-1 Leads United; Meltah Kabiria 1-1 Metro Sports; Zamalek 0-4 TUK; Shauri Moyo Sportiff 2-3 MASA; NYSA 3-1 Tem Umeme; Kayole Asubuhi 1-1 Jericho All Stars; Rongai All Stars 0-2 Makadara Junior League SA