• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kayole Starlets yajipanga kutifua vumbi la kufa mtu

Kayole Starlets yajipanga kutifua vumbi la kufa mtu

Na JOHN KIMWERE

VIONGOZI wa timu ya wanawake ya Kayole Starlets wamevunja kikosi hicho na kusajili upya baadhi ya wachezaji wake pia kunasa wengine wapya kujiweka imara kushiriki kampeni za msimu mpya wa 2020-21. Kayole ni miongoni mwa vikosi 16 ambavyo hushiriki michuano ya Soka la Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL).

Ni miaka mitano sasa tangu Kayole ilipopandishwa ngazi ambapo imekuwa ikiponea chupuchupu kushushwa ngazi isipokuwa mwaka 2017 ilipojikaza kiume na kumaliza katika nafasi ya nne kwenye jedwali la kipute hicho.

“Tunashukuru maana msimu uliyopita tulifanikiwa kusalia katika ligi tulikuwa karibu kuteremshwa ngazi. Tunafuraha kwa hilo ambapo tunapania kurejea kivingine raundi hii tukilenga kubeba ubingwa wa taji la muhula mpya,” amesema kocha wa Kayole, Joshua Sakwa na kuongeza kwamba ukosefu wa fedha ndio umekuwa kizingiti kikubwa kwao bila kuweka katika kaburi la sahau mtindo wa baadhi ya wachezaji wake kulaza damu dimbani.

UKOSEFU WA UFADHILI

Matatizo ya kifedha yalichangia klabu hiyo kusafirisha wachezaji nane hadi mjini Vihiga kushiriki mchezo wa kipute hicho dhidi ya malkia wa soka nchini Vihiga Queens.

”Sijui nini mbaya na wachezaji wangu. Wapo baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa na timu hii kwa muda mrefu ambapo wameonyesha ni kama lazima wasukumwe ili kufanya vizuri angalau kupata matokeo ya kuridhisha ndio maana tumeamua kuvunja timu nzima ili kusajili wachana nyavu wapya,” akasema.

Baada ya kuandaa mechi za majaribio tayari wamenasa saini za wachezaji 15 huku wakiendelea kusaka wachezaji kumi zaidi kusudi kufikisha kikosi cha wanasoka 25. Kati ya idadi ya wanasoka 15 klabu hiyo imerejesha wachezaji saba na kutwaa sura mpya nane. Kocha huyo anasema kuwa wamepania kuunda kikosi imara ili kuonyesha soka la kuvutia kwenye kampeni za msimu ujao.

SAJILI WAPYA

Orodha ya wapigagozi wapya inajumuisha beki wa Harambee Starlets, Juliet Andipo (Thika Queens), beki Foscah Nashivanda na Faith Awuor (kiungo) wote wakitokea Zetech University FC, Faith Atieno (kiungo) kutoka Wadadia LG Mumias, mshambuliaji Josephine Nana kutoka Mathare United Women FC na Clarice Arony (MKU). Wengine wakiwa Sharon Miloya, Fidy Njoki, Hellen Akinyi, Faith Atiero, Leslie Anyango, Faria Ngadira, Hallima Anno, Philistus Awino na Caroline Kamau. Kocha huyo anasema raundi hii wana furaha maana wamenasa kati ya wanasoka mahiri nchini kama Foscah Nashivanda aliyekuwa kati ya kikosi cha Harambee Starlets kiliotwaa taji la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwaka uliyopita.

You can share this post!

MITCHELL WAMBUI: Waliobobea kwa filamu wainue waigizaji...

CHAKICACA: Chama imara kuhusu makuzi ya Kiswahili shuleni...