Michezo

Kazi bado ngumu kwa Harambee Stars baada ya sare na Togo

November 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SARE zilitamalaki mechi za raundi ya pili za kufuzu kwa fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) 2021, siku ya Jumatatu.

Fainali hizo za AFCON 2021 zitakazojumuisha jumla ya vikosi 24, zitaandaliwa nchini Cameroon, ambao awali walikuwa waandae fainali za 2019. Hata hivyo, maandalizi yao ya mwendo wa kobe ulifanya vinara wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwapokonya jukumu hilo na kuipa Misri.

Jumatatu, michuano yote ya Kundi G ilikamilika kwa sare baada ya wanavisiwa wa Comoros kutoshana nguvu na Egypt bila ya kufungana bao lolote. Nao Harambee Stars wa Kenya wakakabwa koo 1-1 na Togo uwanjani MISC Kasarani, Nairobi.

Cape Verde pia walisajili sare ya 2-2 dhidi ya Msumbuji, matokeo sawa yakiandikishwa na Gambia dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Matokeo ya mechi za Kundi G yaliwasaza Comoros kileleni mwa kundi hilo kwa alama nne kutokana na mechi mbili za ufunguzi. Misri na Kenya walioagana kwa sare ya 1-1 mjini Alexandria Alhamisi iliyopita, wanajivunia alama mbili kila mmoja. Togo wanashika mkia kwa pointi moja pekee baada ya kuduwazwa na Comoros kwa kichapo cha 1-0 nyumbani jijini Lome, Alhamisi iliyopita.

Wakicheza dhidi ya Togo saa moja usiku Jumatatu, Stars waliwekwa uongozini na Johanna Omolo kunako dakika ya 37. Hata hivyo, juhudi zilifutwa na Togo dakika ya 64 kupitia kwa Hakim Ouro-Sama.

Licha ya kupata jeraha la kifundo cha mguu katika dakika ya 10, mvamizi Michael Olunga alijituma vilivyo huku ushirikiano kati yake na Victor Wanyama ukichangia bao lililoyumbisha ngome ya Togo.

Huku kocha Francis Kimanzi akiwa mwingi wa sifa kwa vijana wake, Claude Le Roy wa Togo alikataa kujibu mengi ya maswali ya wanahabari. Badala yake aliwalaumu marefa kwa kile alichodai ni maonevu, na kutolewa kwa maamuzi tata dhidi ya kikosi chake.

Japo Kenya ina uwezo wa kuwakomoa Comoros nyumbani na ugenini, mtihani wao mgumu zaidi ni jinsi ya kuwazidi maarifa Togo ugenini na Misri ambao ni mabingwa mara saba wa taji la AFCON.

Katika mchuano wa rtatu, Stars watapepetana na Comoros jijini Nairobi kabla ya kurudiana na kikosi hicho katika mechi yao ya nne. Baadaye, watakuwa wenyeji wa Misri kabla ya kufunga kampeni za makundi kwa kuwaendea Togo jijini Lome. Mechi hizo za raundi za tatu na nne zimeratibiwa kuchezwa kati ya Agosti 31 na Septemba 8 mwaka ujao.

Licha ya Stars kuwekwa katika hilo kundi gumu, Rais wa Shirikisho la Soka nchini (FKF) Nick Mwendwa ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi hicho kitajikakamua vilivyo, na kufuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya pili mfululizo.