KCB kufadhili mafunzo ya makocha wa voliboli
Na GEOFFREY ANENE
BENKI ya KCB imetangaza Jumatatu kufadhili mafunzo ya makocha ya kimataifa ya mpira wa voliboli yatakayofanyika jijini Nairobi mnamo Machi 1-5 kwa kitita cha Sh2 milioni.
Semina hii iliyoidhinishwa na Shirikisho la Voliboli barani Afrika (CAVB), italeta pamoja raia 40 wa kigeni na 30 kutoka Kenya.
Afisa wa KCB wa masuala ya biashara na udhibiti Judith Sidi Odhiambo amesema mafunzo hayo ni muhimu sana katika ukuaji wa michezo barani Afrika.
“Sisi kama KCB Bank Kenya, tunafurahia kuongoza shughuli ya kuinua viwango vya voliboli barani Afrika ili kutuwezesha kushindana vyema na miamba wengine wa voliboli duniani,” alisema Sidi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) Waithaka Kioni aliishukuru KCB kwa kudhamini michezo hasa voliboli katika eneo hili.
“Tunashukuru KCB Bank Kenya kwa kusaidia voliboli kwa miaka mingi. Semina hii ni muhimu kwa makocha wetu ambao wataelimika kuhusu mbinu mpya za ukufunzi pamoja na mifumo,” alisema Waithaka.
Washiriki wanatarajiwa kutua jijini Nairobi mnamo Machi 1 kabla ya ufunguzi rasmi wa warsha hiyo hapo Machi 2 katika ukumbi utakaotumika wa Karen. Mafunzo yenyewe yatakuwa Machi 2-4. Mwalimu wa makocha kutoka Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB) Mauro Berruto kutoka Italia na Rais wa Kamati ya makocha ya CAVB Sherif El Shemerly wataongoza mafunzo hayo ya hali ya juu ya siku tatu.
Makocha watakaopata mafunzo hayo wanatoka katika mataifa ya Kenya, Benin, Botswana, Burundi, Cameroon, Congo, Misri, Malawi, Mauritius, Morocco, Namibia, Nigeria, Rwanda, Senegal, Swaziland, Tanzania, Tunisia na Uganda, miongoni mwa nchi zingine.