KCB kujaribu kurejea kwa ligi kuu
Na CECIL ODONGO
WASHIRIKI wa ligi ya Supa (NSL) KCB huenda wakarejea ligi ya KPL msimu wa 2018/19 baada ya kuwa nyasini kwa misimu mitatu iwapo watashinda mechi moja kati ya mbili zilizosalia za ligi hiyo.
Wanabenki hao wanashikilia nafasi ya pili katika msimamo wa jedwali la NSL na wanahitaji alama tatu katika mechi mbili zilizosalia ili kuandikisha historia kwa kurejea KPL tangu mwaka wa 2015 walipoteremshwa ngazi.
Kocha wa vijana hao Elvis Ayany amekariri kwamba mara hii, timu hiyo itapigana kwa jino na ukucha kuepuka kubanduliwa jinsi ilivyokuwa mwaka wa 2017 huzuni ilipotanda kambini mwao walipokosa kupandishwa ngazi kutokana na kusuasua mechi ya mwisho.
“Tutaendelea kucheza kwa kiwango cha juu ili tupandishwe ngazi msimu huu. Msimu jana mambo yalituendea mrama tulipojikwaa katika mechi ya mwisho na tukakosa kutinga nafasi ya pili. Tulijifunza na msimu huu hatuna budi ila kufunga mikanda hadi sekunde ya mwisho ya msimu,” akasema Ayany.
Vile vile alisema kuwa kikosi chake hakitadharau wala kupuuza wapinzani na kila mechi itakuwa kama fainali kwao.
“Hakuna kudharau mpinzani na kila mechi ni fainali kwetu. Sherehe zitashamiri tukiwa na uhakika kwamba tumefuzu wala hatuna mzaha na mpinzani yoyote,” akasisitiza Ayany.
Iwapo KCB Itashinda, wataungana na Western Stima kujihakikishia marejeo ya KPL. Hata hivyo timu itakayoibukia nafasi ya tatu itashiriki mechi ya mchujo dhidi ya nambari 16 wa KPL kuamua atakayepata tiketi ya mwisho kutinga ligi hiyo.