Kean afungua rasmi akaunti yake ya mabao kambini mwa PSG
Na MASHIRIKA
MWITALIANO Moise Kean alifunga mabao yake mawili ya kwanza kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) na kusaidia miamba hao wa soka ya Ufaransa kuwapepeta Dijon 4-0 uwanjani Parc des Princes.
Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20 aliingia katika sajili rasmi ya PSG mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana na Everton kwa mkopo.
Aliwafungulia PSG ukurasa wa mabao katika dakika ya tatu baada ya kushirikiana na Mitchel Bakker aliyechangia pia mabao mawili yaliyofumwa wavuni na chipukizi Kylian Mbappe katika dakika za 82 na 88 mtawalia.
Kean alicheka na nyavu za Dijon kwa mara ya pili katika dakika ya 23 baada ya kuandaliwa krosi safi na fowadi matata mzawa wa Brazil, Neymar Jr aliyeshuhudia makombora yake mawili katika mechi hiyo yakigonga mwamba wa goli la wageni wao.
Kean alipata jeraha katika dakika ya 73 na nafasi yake kutwaliwa na Mbappe aliyeshirikiana vilivyo na Neymar kuwatatiza mabeki wa Dijon.
Ushindi huo wa PSG, ambao ulikuwa wao wa sita mfululizo kwenye ligi, uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). PSG ya kocha Thomas Tuchel walianza vibaya kampeni za msimu huu wa 2020-21 kwa kupoteza mechi mbili za kwanza.
Dijon kwa sasa wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama mbili kutokana na mechi nane zilizopita.
Mechi ya Ligue 1 iliyokuwa iwakutanishe Lens na wageni wao Nantes uwanjani Bollaert-Delelis mnamo Oktoba 25, 2020 iliahirishwa baada ya wanasoka 11 wa kikosi cha kwanza cha Lens kuugua Covid-19.
Mchuano wa Ligi ya Daraja la Kwanza (Ligue 2) kati ya Grenoble na Nancy pia uliahirishwa kutokana na kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona.