Kenya haitakuwa mteremko dhidi ya Algeria – Migne
Na GEOFFREY ANENE na JOHN ASHIHUNDU
KOCHA Sebastien Migne ameahidi kwamba Kenya haitakuwa mteremko wakati Harambee Stars itavaana na Desert Foxes ya Algeria katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Afrika (AFCON) uwanjani 30 June jijini Cairo mnamo Juni 23, 2019.
Katika mahojiano ya kabla ya mechi hiyo ya Kundi C, Mfaransa Migne ameambia tovuti ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), “Naamini vijana wangu na kesho (Juni 23) tutapigania alama tatu. Hatutakuwa mteremko kwa Algeria.”
Migne aliongoza mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kurejea katika AFCON baada ya kukosa makala ya mwaka 2006, 2008, 2010, 2012, 2013, 2015 na 2017 kwa kumaliza nambari mbili katika mechi za kufuzu za Kundi F nyuma ya Black Stars ya Ghana na mbele ya majirani Ethiopia baada ya Sierra Leone kupigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mwezi Oktoba mwaka 2018 baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia uendeshaji wa soka nchini humo.
Akizungumzia mechi dhidi ya Algeria, nahodha wa Kenya, Victor Wanyama amesema timu iko tayari kuonyesha uwezo wake.
“Tulikuwa na presha wakati wa kufuzu, lakini wakati huu hatuna presha. Ni wakati wetu wa kuonyesha makali yetu,” amesema kiungo huyu anayesakata soka yake ya malipo katika klabu ya Tottenham Hotspur nchini Uingereza.
Kenya itakuwa ikitafuta ushindi wake wa tatu katika mechi nne dhidi ya Waarabu hawa ambao walikubali kichapo cha bao 1-0 mwaka 1997. Walikuwa wamepiga Algeria 3-1 katika mechi nyingine Juni 1 mwaka 1996 kabla ya kunyamazishwa 1-0 wiki mbili baadaye.
Kocha wa Algeria, Djamel Belmadi amekiri kwamba ni vigumu kubashiri mchuano huu, ingawa akaonya Stars “sisi kama Algeria tuko nchini Misri kutwaa taji.”
Mmoja wa wachezaji wakali wa Algeria, ambao Kenya itahitaji kuzima na wakati huo huo ikijitafutia matokeo mazuri ni winga wa Manchester City Riyad Mahrez.
Mahrez, ambaye aliibuka bingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza mwaka 2016 akichezea Leicester City na pia kutawazwa mwanasoka bora wa Bara Afrika mwaka uo huo, amezungumzia mechi ya Kenya akisema, “Hatujawahi kukutana nao kwa muda mrefu. Hata hivyo, tumepata kutazama mechi zao na kupimana nguvu dhidi ya wapinzani wanaocheza kama wao (Burundi). Tutajituma vilivyo kuzoa alama zote tatu.”
Kenya na Algeria ziko katika kundi moja na Senegal na Tanzania ambazo pia zitakabiliana Jumapili.
Akizungumzia mechi kati ya timu yake ya Tanzania na Senegal, nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta amesema, “Hatuangalii yaliyopita. Tutatafuta ushindi.”
Taifa Stars ilikutana na Teranga Lions mara mbili mwaka 2007 katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) na kupoteza 4-0 nchini Senegal na kutoka 1-1 nchini Tanzania.
Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amekiri Senegal ni mpinzani mkali anayejivunia mastaa wengi. Ameongeza, “Itakuwa mechi ngumu sana, ingawa niko na imani katika wachezaji wangu.”
Nahodha wa Senegal, Cheikhou Kouyate amesema, “Joto hapa nchini Misri ni kali sana, lakini halitatuzuia kushinda…”
Naye Kocha Aliou Cisse amesifu Taifa Stars. “Tanzania ni timu nzuri sana. Wana mchezaji Mbwana Samatta ambaye ni mchezaji mzuri sana. Wao hawamtegemei Samatta pekee kwa sababu wako mchezaji mzuri anayeitwa Thomas Ulimwengu na wengineo walio na uwezo wa kudhuru wapinzani. Pia, wana kocha mzuri. Itakuwa mechi ngumu.”
Brian Mandela awasili
Mlinzi matata, Brian Mandela alipokelewa kwa shangwe kwenye kambi ya Harambee Stars nchini Misri baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye goti lake la kulia.
Staa huyo wa klabu ya Maritzburg United aliumia mazoezini nchini Ufaransa kabla ya kikosi hicho cha kocha Sabestien Migne kufunga safari kuja hapa nchini kwa ajili ya michauno ya AFCON na ilibidi aondolewe kikosini.
Mchezaji huyo ametoa shukrani zake kwa Shirikisho la Soka Kenya na wachezaji wenzake kwa kutokana na jinsi walivyoshughulikia maslahi yake.
“Yalikuwa masikitiko makubwa kwangu hasa ikizingatiwa kwamba niliumia siku chache tu kabla ya kuanza kwa michuano yenyewe, lakini nimepata ushauri mkubwa kutoka kila na sasa nimetulia,” alisema Mandela.
“Nitaendelea kuwasapoti kama mshabiki wengine hadi dakika ya mwisho, huku nikiwatakia heri,” aliongeza staa huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye alikuwa katika kikosi kilichoandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Madagascar kwenye mechi ya kirafiki jijini Paris.