Michezo

Kenya Harlequins wajinasia huduma za wanaraga wawili wa kimataifa kutoka Homeboyz RFC

November 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KENYA Harlequins wameimarisha kikosi chao kwa minajili ya kampeni za msimu ujao katika raga ya Kenya Cup kwa kujinasia huduma za wachezaji wawili wa kimataifa Joshua Chisanga na Emmanuel Mavala kutoka Homeboyz RFC.

Chisanga na Mavala walijiunga upya na Homeboyz msimu uliopita baada ya kuwa nje kwa mwaka mmoja wakichezea RC Orkan Sochaczew ya Poland.

Mwenyekiti wa Quins, Michael Wanjala amesema kwamba ujio wa wanaraga hao wawili kambini mwao utaimarisha zaidi kikosi chao na kuinua uthabiti wa kikosi kilichokosa fursa ya kufuzu kwa hatua ya mwondoano mnamo 2019.

“Hawa ni wanaraga wa haiba kubwa watakaoamsha viwango vya ushindani kikosini. Wanaleta nguvu mpya, tajriba pevu na uzoefu mpana utakaotusaidia kusajili matokeo ya kuridhisha katika msimu wa 2020-21,” akasema Wanjala.

Quins walikamilisha kampeni za mwaka wa 2019-20 katika nafasi ya tisa baada ya kujizolea jumla ya alama 28 ambapo walisajili ushindi mara tano na kupoteza jumla ya michuano 11.

Chisanga na Mavala wanajiunga na mwanaraga mwingine wa zamani wa Homeboyz, Mark Wandetto aliyeingia katika sajili rasmi ya Quins mnamo Mei 2020.

Wandetto alikuwa miongoni mwa wanaraga tegemeo katika timu ya taifa ya Shujaa chini ya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Paul Murunga. Alikuwa mchezaji wa pili baada ya Leroy Mbugua kutoka Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kusajiliwa na Quins muhula huu. Wandetto alikuwa mhimili wa Homeboyz kwa misimu miwili iliyopita.

Wanjala pia amefichua kwamba wanalenga kukamilisha usajili wa mchezaji Philip Ikambili kutoka Homeboyz na wanaraga wengine wawili wa USIU-A.

Licha ya kwamba serikali bado haijaidhinisha kurejelewa kwa michezo ya kugusana katika mojawapo ya hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, Quins wamekuwa wakijiandaa kwa msimu ujao wa 2010-21.

“Hatuwezi kupumzika. Lazima tupangie vyema kampeni za muhula ujao licha ya changamoto tele ambazo zimezuliwa na Covid-19. Benchi ya kiufundi inajitahidi kukisuka upya kikosi kwa minajili ya muhula ujao na tunajiandaa kutambulisha rasmi wanaraga wapya waliojiunga nasi kwa mashabiki,” akaongeza Wanjala kwa kusisitiza kwamba Quins wamerefusha mkataba wao na kampuni ya Samurai Sportswear itakayowadhamini kwa miaka mingine mitatu ijayo.

Quins wanajivunia idadi kubwa ya wanaraga chipukizi ambao wanalenga kuwakweza kutoka akademia hadi kikosi cha kwanza. Baadhi yao ni nahodha wa kikosi cha vijana wasiozidi umri wa miaka 20 Boniface Ochieng, Elisha Koronya na Melvin Thairu waliokuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande, Simbas mnamo 2019.