Kenya kusaka tiketi ya CHAN 2020 dhidi ya Burundi
Na GEOFFREY ANENE
KENYA itamenyana na Burundi katika jaribio lake la sita la kutafuta tiketi ya kuwa mmoja wa washiriki wa soka ya Bara Afrika kwa wachezaji wanaosakata katika mataifa yao (CHAN) mwaka 2020.
Droo ya mechi za kufuzu kushiriki kombe la mwaka 2020 ilifanywa jijini Cairobi nchini Misri mnamo Januari 30, 2019.
Harambee Stars ilijaribu kuingia makala ya mwaka 2009, 2011, 2014 na 2016 bila mafanikio, na ilipofuzu kama mwenyeji mwaka 2018, Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) liliipokonya haki za kuandaa mashindano haya kutokana na ukosefu wa viwanja pamoja na vifaa vingine, huku hali ya usalama pia ikichangia.
Mataifa 47 yatawania tiketi 15 zilizoko mezani ili kuungana na Ethiopia iliyofuzu moja kwa moja kama wenyeji. Mechi za kufuzu zitatumia mfumo wa maeneo (zoni).
Eneo la Afrika Mashiriki litajumuisha mataifa manane – Kenya, Uganda, Tanzania, Sudan, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Somalia. Yatapigania tiketi mbili zilizotengewa eneo hili.
Kenya itapepetana na Burundi katika raundi ya kwanza. Mataifa haya yanafahamiana sana kutokana na kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati almaarufu CECAFA Cup pamoja na mechi kadhaa za kirafiki.
Kenya inajivunia kuchapa Burundi 1-0 zilipokutana mara ya mwisho mwaka 2017 katika CECAFA Cup, ambayo Kenya iliandaa na pia kutwaa taji.
Stars na Swallows ya Burundi ziliwahi kukutana katika mechi ya kufuzu kushiriki CHAN mwaka 2014. Burundi ilibandua Kenya nje kwa jumla ya bao 1-0 baada ya kuichapa 1-0 nchini Burundi na kulazimisha sare tasa jijini Nairobi.
Wakifaulu kuzima Burundi, vijana wa kocha Sebastien Migne watakabiliana na Tanzania ama Sudan katika raundi ya pili. Mshindi wa raundi ya pili ataingia CHAN 2020. Tarehe za kuanza kushindania tiketi za kufuzu bado hazijatangazwa.