Kenya kutuma maafisa wa serikali London Marathon
ELIAS MAKORI na GEOFFREY ANENE
KENYA itatuma msafara wa maafisa wa ngazi ya juu serikali kwenye mbio za kifahari za London Marathon za mwaka 2020 mnamo Oktoba 4 nchini Uingereza.
Katika mahojiano Septemba 18, Katibu wa Michezo Joe Okudo alisema kuwa viongozi hao watakuwepo kupatia wakimbiaji kutoka Kenya motisha ya kung’ara katika makala hayo ya 40.
Yatafanyika bila mashabiki na pia kuhusisha watimkaji maarufu pekee katika eneo la St James’s Park ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona ambavyo vimeua watu 6,885 jijini London pekee na 36,765 nchini Uingereza.
Okudo alisema kuwa mipango ya ziara hiyo inakaribia kukamilishwa.
“Waziri wa Michezo (Amina Mohamed) ataongoza msafara wa viongozi kutoka Kenya watakaosafiri hadi London mara tu shindano la Kip Keino Classic litakapokamilika (jijini Nairobi) Oktoba 3. Tunamaliziamalizia mipango hiyo,” Okudo alisema.
Serikali inalenga kutumia mbio za London Marathon na Kip Keino Classic kunadi Kenya kama nchi ambayo sasa iko tayari kwa biashara baada ya kuvurugwa na janga la virusi vya corona.
Tayari, Wizara ya Utalii na Wanyamapori imetwika bingwa wa London Marathon mwaka 2015, 2016, 2018 na 2019 Eliud Kipchoge majukumu ya Balozi wa Kenya.
Mwaka 2019, Naibu Rais William Ruto alikuwa katika eneo la kumalizia mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge. Kipchoge alitimka mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 1:59:40 mjini Vienna nchini Austria na kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha umbali huo chini ya saa mbili.
Mbio za London Marathon 2020 zinasubiriwa kwa hamu kubwa, hasa kwa sababu pia zitakutanisha mahasimu Kipchoge na Muethiopia Kenenisa Bekele, ambao wanajivunia kasi ya juu katika ukimbiaji wa kilomita 42.
Kipchoge anashikilia rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 aliyoweka Berlin Marathon 2018 nchini Ujerumani naye Bekele alikosa rekodi hiyo kwa sekunde mbili akishinda mjini Berlin mwaka 2019.
Mbio za London Marathon zitahusisha wakimbiaji 45 wanaume pamoja na wawekaji kasi nane akiwemo Sir Mo Farah katika kitengo hicho.
Idadi hiyo inatarajiwa katika kitengo cha kinadada ambapo kuna Wakenya Brigid Kosgei (bingwa mtetezi), Ruth Chepng’etich, Vivian Cheruiyot, Valery Jemeli na Edith Chelimo. Wakenya Pauline Kamulu, Sandrafelis Chebet, Lydia Mathathi na Nancy Jelagat wako katika orodha ya wawekaji kasi wa kitengo hiki.