Kenya kuvaana na UG bila Wanyama, Omollo na Okumu
Na CHRIS ADUNGO
TIMU ya taifa ya Harambee Stars imepania kuimarisha zaidi maandalizi yake kwa minajili ya mchuano wa kirafiki utakaowakutanisha na majirani Uganda Cranes uwanjani MISC Kasarani mwishoni mwa wiki hii.
Chini ya mkufunzi mpya Francis Kimanzi, Stars watapania kutumia mchuano huo kama sehemu ya mikakati ya kujiandaa kwa kivumbi cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 nchini Cameroon.
Kwa Uganda, mechi hiyo itawapa jukwaa la kujinoa kwa mchujo wa mikondo miwili ya kufuzu kwa CHAN 2020 dhidi ya Burundi na AFCON 2021.
Stars wamepangwa kuvaana na Misri ugenini mnamo Novemba 2019 katika mechi hiyo ya kwanza ya Kundi G linalowajumuisha pia Togo na Comoros.Kabla ya kuvaana na Misri waliokuwa wenyeji wa fainali za AFCON mwaka huu, Stars watapangiwa michuano mingine miwili ya kirafiki. Watapepetana na Libya mnamo Oktoba 10, 2019 kabla ya kupimana nguvu na Morocco au mabingwa wa AFCON 2004, Tunisia.
Watakapocheza na Uganda, Stars watakosa huduma za nahodha Victor Wanyama, kiungo Johanna Omollo na beki Joseph Okumu ambaye alijiunga majuzi na IF Elfsborg ya Uswidi. Kwa mujibu wa Kimanzi, Okumu anauguza jeraha. Wanyama alitarajiwa kubanduka Tottenham na kurejea Celtic ya Scotland kwa mkopo.
Abdallah Mubiru ambaye ni kocha mpya wa timu ya Uganda amekitaja kikosi chake cha mwisho kitakachoondoka jijini Kampala mnamo Alhamisi wiki hii kuelekea Nairobi.
Katika jitihada za kujaza pengo kocha Sebastien Desabre aliyeagana nao mwishoni mwa fainali za AFCON 2019, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) linatarajiwa kutaja benchi rasmi la kiufundi mnamo Alhamisi wiki hii.
Mechi hizo zitakuwa za kwanza kusimamiwa na kocha Kimanzi aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Mfaransa Sebastien Migne ambaye mkataba wake ulitamatishwa na FKF Julai 2019.
Kibarua kizito
Kimanzi alitaja kikosi cha wanasoka 24 aliowaita kambini kuanza mazoezi kwa ajili ya kibarua kizito na kigumu dhidi ya Cranes. Wengi wa wachezaji aliowajumuisha katika kikosi hicho ni wale waliowakilisha nchi katika fainali za AFCON 2019 huku akimrejesha pia mshambuliaji matata wa Zesco United ya Zambia, Jesse Jackson Were.
Kadhalika, kocha huyo wa zamani wa Mathare United na Tusker alimuita kambini kiungo Moses Mudavadi wa Kakamega Homeboyz, mbali na kuwataja wachezaji wengine 10 wa akiba ambao wanaweza kujumuishwa katika kikosi cha Stars wakati wowote.
Makipa: Patrick Matasi (St George SC, Ethiopia), John Oyemba (Kariobangi Sharks) na Faruk Shikalo (Young Africans SC, Tanzania).
Mabeki: Mike Kibwage (KCB), Joash Onyango (Gor Mahia), Bernard Ochieng (Wazito), Aboud Omar (Sepsi OSK Sfantu Gheorghe, Romania), Erick Ouma (Vasalunds IF, Uswidi), Nicholas Meja (Bandari), Samuel Olwande (Kariobangi Sharks).
Viungo: Victor Wanyama (Celtic, Scotland), Francis Kahata (Simba SC, Tanzania), Boniface Muchiri (Tusker), Kenneth Muguna (Gor Mahia), Duke Abuya (Kariobangi Sharks), Ismael Gonzales (UD Las Palmas FC, Uhispania), Cliffton Miheso (Gor Mahia), Ayub Timbe (Beijing Renhe FC, China), Cliff Nyakeya (FC Masr, Misri), Erick Johanna (IF Brommapojkarna, Uswidi), Moses Mudavadi (Kakamega Homeboyz), Whyvone Isuza (AFC Leopards), Lawrence Juma (Gor Mahia).
Wavamizi: Michael Olunga (Kashiwa Reysol FC, Japan), Jesse Were (Zesco United, Zambia), John Avire (Sofapaka FC, Kenya), Enosh Ochieng (Ulinzi Stars).